Habari
TANZANIA NA URUSI ZASAINI VIPENGELE VYA MFUMO WA MAKUBALIANO YA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA BIASHARA
Tanzania na Urusi zasaini vipengele vya mfumo wa makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa Biashara na Uchumi wakihitimisha Mkutano wa kwanza wa tume ya pamoja ya Ushirikiano wa Biashara na Uchumi baina ya nchi zao, leo jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wa siku mbili umehusisha; Mkutano wa Wataalamu, Mkutano wa Tume ya pamoja na Kongamano la Uwekezaji, kabla ya kuhitimishwa kwa ngazi ya juu ya Waheshimiwa Mawaziri kutia saini makubaliano hayo.
Katikatika taarifa yao waliyoitoa kwa pamoja mara baada ya kutia saini makubaliano hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb), na Mhe. Maxim Reshetnikov, Waziri wa Urusi anayeshughulikia Maendeleo ya Kiuchumi, wamethibitisha kuwa nchi zao zinachukua mkondo wa uhusiano wa biashara na uchumi.
Mhe. Prof. Mkumbo amesema miongo sita ya uhusiano wa Tanzania na Urusi imekuwa imara kisiasa na kiutamaduni, ikileta manufaa makubwa katika elimu, sayansi na teknolojia.
Hivyo, majadiliano ya kuimarisha uhusiano wa biashara na uchumi yanalenga kupanua wigo kwa kuimarisha ushirika wa kiuchumi hususani katika sekta za; Viwanda na Biashara, fedha, nishati, kilimo, na elimu, sayansi na teknolojia, uchukuzi, afya na Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Kwa Mujibu wa Mhe. Prof. Mkumbo, maliasili na Utalii, utamaduni na michezo ni maeneo mengine ya sekta za ushirikiano miongoni mwa makubaliano yaliyotiwa saini.
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Urusi Mhe. Maxim Reshetnikov amesema Urusi inaitambua Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa ambayo uchumi wake unaimarika katika nyanja mbalimbali, hivyo shabaha yao ni kuifanya Tanzania kuwa Mshirika wa kimkakati wa masuala ya Biashara na Uchumi katika ukanda wa Afrika.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Pindi Chana, Naibu Waziri wa Viwanda, Mhe. Exaud Kigahe, Mhe, Injinia Meryprisca Mahundi, ni miongoni mwa wageni mbalimbali waliohudhuria mkutano huo.
Mkutano wa kwanza wa kamati ya wataalamu baina nchi hizo uliyoongizwa jana na Katibu Mkuu Dkt. Tausi Mbaga Kida kwa upande wa Tanzania na Bwa. Pavel Kalmychek Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Uwili, Wizara ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Shirikisho la Urusi.