Habari
DKT. CHAYA AIPONGEZA AVOAFRICA KWA KUTATUA CHANGAMOTO YA SOKO LA PARACHICHI
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Chaya, ameipongeza Kampuni ya Avoafrica TZ Limited kwa kuwekeza katika uchakataji wa parachichi na kutoa suluhisho la changamoto ya wakulima kukosa soko la uhakika, hususan kwa parachichi yanayoshindwa kufikia viwango vya masoko ya kawaida na kuharibika baada ya kuvunwa.
Dkt. Chaya ametoa pongezi hizo alipotembelea kiwanda cha kampuni hiyo kilichopo Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, kinachojishughulisha na uzalishaji wa mafuta yatokanayo na parachichi. Amesema uwekezaji huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 25 ni mfano wa ubunifu unaoongeza thamani ya mazao ya kilimo, kupunguza upotevu na kuwawezesha wakulima kupata kipato. Ameipongeza pia Serikali ya Mkoa wa Njombe, chini ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Anthony Mtaka, kwa juhudi za kuvutia uwekezaji huo.
Kiwanda hicho kilichoanza shughuli zake Januari 2025 kina uwezo wa kuchakata tani 400 za parachichi ndani ya saa 24 na kuzalisha tani 30 za mafuta, sawa na lita 32,800.
Dkt. Chaya amesema Serikali itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto za wawekezaji, ikiwemo miundombinu ya barabara, huduma za ugani, uhifadhi wa mabaki ya uzalishaji na upatikanaji wa maji kupitia kilimo cha umwagiliaji, ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji.
Kwa mujibu wa taarifa ya kampuni, mwaka 2025 ilinunua tani 20,000 za parachichi zenye thamani ya Shilingi bilioni 20, huku mwaka 2026 ikitarajia kununua tani 23,000 zenye thamani ya Shilingi bilioni 21. Ununuzi huo unanufaisha zaidi ya wakulima 4,000 kutoka mikoa mbalimbali nchini ikiwemo kwa kuwapatia soko la uhakika, hususan kwa parachichi ambazo awali zingeweza kuharibika kutokana na kutokidhi viwango vya masoko ya kawaida.
Aidha, uwekezaji huo umewezesha upatikanaji wa ajira za moja kwa moja 300 na 400 wakati wa msimu, na ajira zisizo za moja kwa moja kwa zaidi ya watu 500.
