Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

PROF. MKUMBO ASISITIZA UMUHIMU WA TASAF KUWA TAASISI KUU YA KUPAMBANA NA UMASKINI NCHINI TANZANIA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ameitaka Menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuharakisha mchakato wa kuifanya kuwa taasisi wa kupambana na umaskini nchini ili kuongeza ufanisi, uratibu na uendelevu wa programu zinazolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Prof. Mkumbo ameyasema hayo Oktoba 20, 2026 jijini Dodoma, wakati wa kikao na Menejimenti ya TASAF na kujadili namna bora ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika mapambano dhidi ya Kunusuru Kaya Maskini. Amesisitiza umuhimu wa kujifunza kutokana na uzoefu wa programu zilizopita, kuimarisha ufuatiliaji na tathmini, pamoja na kufanya utafiti wa mifumo inayotumika katika nchi mbalimbali ili kubaini njia zinazofaa zaidi kwa Tanzania.

Aidha, ameelekeza kuwa utafiti huo na mapendekezo ya mfumo unaofaa yakamilishwe kabla ya mwisho wa mwaka 2026, ikiwemo kutathmini uwezekano wa kuanzisha taasisi kuu maalumu au kutumia taasisi zilizopo kusimamia programu hizo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Shadrack Mziray, amesema programu za TASAF zinalenga kuongeza uzalishaji vipato vya kiuchumi, kuweka akiba, kuwekeza ili kukuza na kujenga ustawi wa kaya kama sehemu ya mkakati mpana wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini.

Naye Mchumi Mwandamizi na Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Bi. Claudia Zambra, amesema kuna jitihada za kuboresha mbinu za kutambua kaya maskini kwa kuzingatia umiliki wa mali kwa matumizi ya kaya. Ameongeza kuwa kuimarisha mifumo ya kijamii, ikiwemo kanzidata ya kaya (Social Protection Registry), kutasaidia kutambua kaya zenye uhitaji, kurahisisha utoaji wa huduma na msaada wakati wa majanga, pamoja na kuongeza ustahimilivu wa kaya na mchango wa programu hizo katika kupunguza umaskini.

Kikao hiki kimehudhuriwa pia na Dkt. Pius Chaya, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Mursali Milanzi, Naibu Katibu Mtendaji - Mipango ya Kitaifa kutoka Tume ya Taifa ya Mipango pamoja, wakuu wa idara na vitengo wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji; pamoja na Menejimenti ya TASAF.