Habari
DKT. KIDA NA MKUU WA IDARA YA AFRIKA MASHARIKI YA UHOLANZI WAKUTANA NA KUJADILI SHUGHULI ZA UBORESHAJI WA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI NA BIASHARA

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Afrika Mashariki wa Uholanzi Bi. Sanne Lowenhardt pamoja na Mshauri Maalum kuhusu Africa wa Wizara hiyo Bw. Melle Leenstra.
Katika mazungumzo yao, Dkt. Kida alibainisha namna Serikali ya Tanzania inavyoendelea kuchochea mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini kupitia falsafa ya 'R Nne' iliyoasisiwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akitaja baadhi ya mageuzi hayo, Katibu Mkuu amesema kuwa pamoja na mambo mengine, eneo mahususi ni Maboresho ya mazingira ya Uwekezaji na Biashara nchini ili kuvutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni ikiwemo Uholanzi hasa kwa kuzingatia umuhimu wa nchi hiyo kwa Tanzania.
Mbali na maboresho ya mazingira ya Uwekezaji na Biashara yanayoendelea nchini, Dkt. Kida aligusia umuhimu wa Mkakati wa nchi ya Uholanzi kwa Afrika (The Africa Strategy of the Netherlands 2023 - 2032).
"Mkakati wenu umekuja kipindi muafaka sana kwa nchi yetu, mnafahamu tunaandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo Mikakati ya nchi za kimkakati kwa Tanzania ikiwemo Uholanzi na nchi za Ulaya litazingatiwa" Alieleza Dkt. Kida.
Wakitoa uzoefu wa Nchi yao katika maboresho ya mazingira ya Uwekezaji na Biasha, Bi. Lowenhardt na Bw. Leenstra walimwambia Dkt. Kida kuwa Uholanzi imefanikiwa kwa kuweka Mifumo, Sera na Mikakati mizuri inayotabirika na kuwafanya wawekezaji wawe na imani kwa serikali ili waamue kuwekeza.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania Nchini Uholanzi, Mhe. Caroline Chipeta aliishukuru nchi ya Uholanzi kwa kuendelea kuenzi Uhusiano wa kidiplomasia uliodumu kwa muda mrefu baina ya Tanzania na Uholanzi ambapo Tanzania imenufaika na mahusiano hayo katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Tanzania imeendelea kuimarisha mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kwa kuitambua na kuipa nafasi kwa kuwa ni wadau muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi.