Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

SERIKALI YACHUKUA HATUA MBALIMBALI ZA KUIMARISHA USTAHIMILIVU WA UCHUMI WA TAIFA: PROF. MKUMBO


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amehudhuria na kufungua kikao kazi cha   kutathmini  athari za kiuchumi kwa Tanzania zitokanazo na mgogoro unaoendelea katika Mashariki ya Kati, kati ya Marekani na Iran. Kikao hicho kimefanyika jijini Dar es Salaam kikishirikisha viongozi wa Serikali, wataalamu wa uchumi, sekta binafsi pamoja na taasisi za kimataifa.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria kikao hicho ni Katibu Mkuu wa Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Mbaga Kida; Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bi. Susan Ngongi Namondo; Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania, Bw. Shigeki Komatsubara; Manaibu Katibu Watendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Mursali Milanzi; Dkt. Blandina Kilama, Bw. Sosthenes Kewe; na  Mchumi Mkuu wa UNDP, Kanda ya Afrika, Bw. Raymond Gilpin.

Katika hotuba yake, Prof. Mkumbo amesema mgogoro huo unaweza kuathiri uchumi wa Tanzania kupitia kupanda kwa bei ya mafuta, gharama za usafirishaji, uzalishaji pamoja na mfumuko wa bei kutokana na utegemezi wa nchi katika uagizaji wa mafuta kutoka mataifa ya Gulf.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha ustahimilivu wa uchumi wa Taifa ikiwemo kuimarisha uwekezaji katika nishati mbadala, kuongeza ushirikiano wa kikanda na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo na uwekezaji.

Amesema, pamoja na athari hizo bado Tanzania ipo pazuri kutokana na kuwa inajiyoshereza kwa chakula na uchumi wake unajengwa na vyanzo mbalinbali vya kiuchumi.