Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

SERIKALI YAENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAWEKEZAJI. DKT. CHAYA


Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, amesema Serikali inatekeleza hatua za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Tanzania (MKUMBI II), ikiwemo kupunguza utitiri wa tozo, kodi na ukaguzi unaofanywa na taasisi mbalimbali.

Akizungumza Julai 30, 2026 baada ya kutembelea Kiwanda cha vifungashio cha Harsho Packaging kilichopo Hai, mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Chaya amesema ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni lazima Serikali ibadili mfumo wa utendaji na kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi.

"Lazima twende na business unusual, tufanye vitu visivyo vya kawaida. Tukiona mtu ana mtaji tumlee. Kupitia MKUMBI II tunaenda kupunguza utitiri wa tozo na kodi, pamoja na kutengeneza mfumo mmoja wa ukaguzi wa taasisi za udhibiti," amesema Dkt. Chaya.

Amesema mfumo huo utapunguza usumbufu kwa wawekezaji ambao kwa sasa hukaguliwa na taasisi mbalimbali zenye majukumu yanayofanana.