Habari
DKT. MPANGO AWATAKA WAWEKEZAJI KUTOA MAONI KUHUSU KODI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ikiwemo kuimarisha hali ya ulinzi, amani na usalama na kuboresha mfumo wa viwango vya kodi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Kongamano la Kodi na Uwekezaji la Mwaka 2025 linalofanyika leo tarehe 15 Aprili, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Ametoa rai kwa washiriki wa Kongamano hilo kujielekeza katika kuibua mawazo na mikakati mipya itakayowezesha Taifa kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani na hivyo kuiwezesha Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi na kupunguza utegemezi kwa wahisani.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kutumia vema fursa inayotolewa na Serikali kila mwaka kutoa maoni na kuwasilisha mapendekezo yao ya kuboresha sera za kodi na uwekezaji kwa kuchangia moja kwa moja katika jukwaa hilo au kupitia dirisha la kidigitali. Pia amewaagiza Mawaziri wa kila sekta kutoa maoni ya kuongeza mapato ya ndani katika sekta zao na kuhakikisha kuwa maoni na mapendekezo yatakayotolewa na wadau kwa njia mbalimbali yanafanyiwa kazi bila kudumaza ukuaji wa sekta husika.
Makamu wa Rais amesema zipo hatua mbalimbali zinazopaswa kutekelezwa zinazoweza kuongeza mapato ya ndani ikiwemo kuweka mkazo zaidi katika kuimarisha uwezo wa ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya ndani, kuongeza jitihada katika kuboresha mfumo wa kodi ambao utahakikisha usawa na kuondokana na misamaha ya kodi isiyo na tija pamoja na kutoa vivutio vya kutosha kwa mawakala na taasisi za kukusanya kodi na kukabiliana na vitendo vya rushwa.
Makamu wa Rais amelitaka Kongamano hilo kufanya tafakuri ya kina na kuainisha maboresho yanayohitajika kisera, kisheria, kikanuni na kiutaratibu ili kuwezesha uwekezaji na biashara na hivyo kuleta mageuzi makubwa katika mfumo wa kikodi na ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Saada Mkuya amesema Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango wa Sekta Binafsi katika uwekezaji na hivyo imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini kupitia utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara nchini ili sekta binafsi iweze kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa Taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Stanslaus Haroon Nyongo (Mb) amesema kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa lengo la kuwawezesha Watanzania na wageni kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi nchini kwa kufanya mapitio ya jumla ya sheria 66 za kisekta.
Mhe. Nyongo ameongeza kuwa mwaka 2019, Serikali ilianzisha na kupitisha Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini (MKUMBI) kwa lengo la kurahisisha taratibu za udhibiti, kuondoa mwingiliano wa majukumu kati ya taasisi mbalimbali za Serikali, pamoja na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji huduma kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini Bi. Angelina Ngalula amesema ni vema elimu sahihi kuendelea kutolewa kwa wafanyabiashara ili waweze kurasimisha biashara zao hali itakayopelekea waweze kupata faida za mikopo na ufadhili na hivyo serikali kuongeza wigo wa ukasanyaji kodi.
Ameongeza kwamba, jitihada lazima zifanyike kupitia vitengo vya utafiti vya Wizara kuhakikisha elimu inapatikana kwa wafanyabiashara ili kuondokana na idadi ndogo ya walipa kodi ambao ni milioni mbili waliopo hivi sasa.
Kongamano hilo linashirikisha viongozi wa Serikali, wadau mbalimbali wa sekta binafsi, wafanyabiashara na wawekezaji. Kauli mbiu ya Kongamano hilo ni "Kuongeza ukuzaji wa rasilimali za ndani kupitia kustawisha fursa za wananchi"