Habari
PROF. MKUMBO ATUNUKIWA TUZO YA KUTAMBUA UONGOZI MAHIRI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mb.), ametunukiwa tuzo maalum na Baraza la Wafanyakazi wa ofisi hiyo kama ishara ya kutambua uongozi wake mahiri na mchango mkubwa katika kusimamia ajenda za maendeleo ya taifa.
Kabla ya kukabidhi tuzo hiyo, Katibu Mkuu Dkt. Tausi Kida, alieleza kuwa Prof. Mkumbo ameonesha uongozi wa mfano kwa kutoa miongozo mbalimbali ambayo wakati wote iliisaidia Ofisi yake kutatua changamoto ilizokabiliana nazo na kufanikiwa kutekeleza majukumu ya Ofisi hiyo.
Katibu Mkuu Dkt. Kida amesema kuwa Prof. Mkumbo amekuwa akibeba na kutafasiri maono ya kitaifa kwa ufanisi mkubwa na kusaidia kutoa uongozi akitolea mfano kukamilika kwa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na kusimamia kwa mafanikio uwekezaji wa sekta binafsi na umma.
“Katika kipindi cha uongozi wako, miradi ya uwekezaji imeongezeka kwa kiwango kikubwa, sambamba na ongezeko la mtaji na ajira nchini,” alisema Dkt. Kida.
Aidha, Dkt. Kida alieleza kuwa Prof. Mkumbo aliongoza usimamizi wa utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI), ambao umeleta mageuzi makubwa kwa kupunguza tozo zisizo na tija, kuunganisha taasisi zenye majukumu yanayofanana, na kuweka mifumo ya kielektroniki ya utoaji huduma kwa wawekezaji na wafanyabiashara.
Akiwa mwenye furaha, mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Prof. Mkumbo alisisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya uongozi na watumishi wa ofisi hiyo, akiwahimiza kuendelea kushirikiana kwa bidii katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Tuzo hiyo iliyotolewa wakati wa Kikao cha tatu cha Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, kilichofanyika tarehe 28 Mei 2025.
Tuzo hiyo ni ushuhuda wa uongozi bora wa Prof. Mkumbo katika kusimamia mipango na uwekezaji, na inaonesha jinsi ambavyo juhudi zake zimeleta matokeo chanya katika maendeleo ya taifa.