Habari
PROF. MKUMBO AFANYA ZIARA KIWANDA CHA KILOMBERO SUGAR (K4) KILICHOPO MOROGORO
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Alexander Mkumbo akiwa ziarani kutembelea Kiwanda cha Sukari cha Kilombero (K4) kilichopo Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.
Kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha tani 260,000 za sukari kwa mwaka na kutoa ajira zaidi ya 900,000. Akizungumza na vyombo vya habari, Mhe. Prof. Mkumbo amewataka wakazi wa Kilombero kuupokea na kuuenzi uwekezaji huo kwa kushirikiana vyema na wawekezaji ili kujenga mahusiano chanya yatakayozalisha manufaa kwa pande zote.
Aidha, ameahidi kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwa bega kwa bega na wananchi pamoja na kuhamasisha uwekezaji zaidi nchini.
“Nia yetu ni kuhakikisha uwekezaji unazalisha ajira kwa vijana wetu. Tunajenga viwanda vikubwa kama hiki, ambacho ni miongoni mwa vikubwa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, kwa lengo la kukuza uchumi wa Tanzania kufikia dola za Marekani trilioni 1 ifikapo mwaka 2050,” amesisitiza Mhe. Prof. Mkumbo.
