Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

PROF. MKUMBO ATOA MWELEKEO MPYA: SEKTA BINAFSI KUWA NGUZO YA UCHUMI WA TAIFA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo leo tarehe 15 Aprili,2026 amekutana na wadau wa Sekta Binafsi katika kikao maalum kilicholenga kutambulisha rasmi mabadiliko ya kimuundo ya wizara yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo Sekta Binafsi sasa itasimamiwa na Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.

Katika hotuba yake, Waziri alieleza kuwa mabadiliko hayo yamepanua wigo wa majukumu ya Ofisi, kwa kuingiza maeneo muhimu yatakayochochea kasi ya maendeleo ya uchumi, ikiwa ni pamoja na uratibu na usimamizi wa maendeleo ya sekta binafsi, usimamizi wa mauzo ya nje (export), pamoja na utekelezaji wa programu maalum ya kuondoa umaskini.

Alisisitiza kuwa jukumu lake kuu litakuwa kuhakikisha kunakuwepo mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji, sambamba na kujenga sekta binafsi imara na yenye uwezo wa kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.

Aliongeza kuwa Serikali inatambua changamoto zilizokuwepo kwa muda mrefu katika sekta hiyo, na iko tayari kushughulikia kwa kushirikiana na wadau kupitia mbinu ya co-creation of solutions, huku akisisitiza umuhimu wa mageuzi (reforms) na uwajibikaji wa pande zote mbili — Serikali na sekta binafsi.

Akitoa maoni kwa niaba ya wafanyabiashara, mwakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania alimpongeza Waziri kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kushirikiana na sekta binafsi, huku akiomba kuwepo kwa majukwaa ya pamoja yatakayohusisha wizara mbalimbali ikiwemo TAMISEMI, Fedha, Uchukuzi na Mambo ya Ndani ya Nchi ili kurahisisha uratibu na maamuzi ya kisera.

Aidha, alieleza kuwa bado kuna vikwazo vinavyokwamisha ukuaji wa sekta binafsi, ikiwa ni pamoja na baadhi ya watendaji wanaofanya kazi kwa mazoea, pamoja na ugumu wa upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za fedha kutokana na masharti magumu ya kibenki.