Habari
Prof. Mkumbo atembelea kiwanda kipya na kikubwa zaidi cha sukari katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini cha Kilombero Sugar Company.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ametembelea kiwanda kipya na kikubwa zaidi cha sukari katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini cha Kampuni ya Kilombero kinachojulikana kama Kilombero Four Sugar.
Kiwanda hicho kimejengwa kwa uwekezaji wa jumla ya Shilingi bilioni 700, na kinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa sukari kwa pamoja hadi tani 270,000 kwa mwaka kutoka katika viwanda vyote vya Kilombero Sugar. Kwa sasa, kampuni hiyo huzalisha takribani tani 130,000 za sukari kwa mwaka.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika tarehe 24 Februari 2026, Prof. Mkumbo alisema lengo la ziara yake lilikuwa ni kujiridhisha kuwa yale yaliyoandikwa kwenye makubaliano na nyaraka za uwekezaji yanatekelezwa kwa vitendo.
Prof. Mkumbo alielezea kufurahishwa kwake na uongozi wa Kilombero Sugar kwa kutekeleza kikamilifu makubaliano yaliyosainiwa.
Aidha, alisema ameridhishwa na namna kampuni hiyo inavyoajiri vijana wazawa wa Tanzania waliohitimu katika vyuo vikuu hapa nchini katika maeneo mbalimbali, kuanzia uhandisi hadi idara za usaidizi.
“Nimefurahi kuona vijana hawa wa kike na wa kiume, wenye vipaji na waliohitimu masomo yao katika vyuo vyetu vikuu wakifanya kazi hapa. Na ninaambiwa kiwanda hiki kitaajiri wafanyakazi 900,000” alisema Prof. Mkumbo na kuongeza;
"Kiu ya Serikali katika kuongeza ajira zinaanza kuonekana, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira 2050, ambayo inalenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2050 angalau asilimia 50 ya Watanzania milioni 118 watakuwa na ajira zenye staha"
Kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero,. Dunstan Kyobya alimpongeza Waziri Mkumbo kwa kuwa waziri wa kwanza kutembelea Wilaya hiyo tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu.
Kyobya alisema kuwa mara baada ya kiwanda cha Kilombero 4 kuanza uzalishaji mwezi Juni mwaka huu, kinatarajiwa kumaliza tatizo la upungufu mkubwa wa sukari nchini Tanzania huku kikidhi soko la miwa wilayani humo.
Kwa sasa, kampuni ya Kilombero Sugar ina viwanda vitatu vya uzalishaji sukari; K1, K2 na K4i, wakati K3 huzalisha ethanol. Umiliki wa kampuni hiyo ni asilimia 75 na 25 kwa wawekezaji na Serikali, mtawalia.
