Habari
PROFESA MKUMBO ATOA WITO KWA WADAU KUTOA MAONI MKUMBI II

Serikali imetoa wito kwa wadau wa sekta ya biashara na uwekezaji kuchangia maoni katika maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II).
Wito huo ulitolewa Juni 06, 2025, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Prof. Mkumbo alieza kuwa, Timu ya Kitaalamu ya Kitaifa imekamilisha hatua za awali na sasa inatarajiwa kuanza kukusanya maoni kutoka kwa wadau katika mikoa 16 nchi nzima kuanzia wiki ijayo.
“Tunataka kuchukua maoni ya wadau wengi zaidi, kama tulivyofanya katika Dira ya Taifa 2050 ili tupokee changamoto za mazingira ya biashara yaliyo, na kuleta Mpango ambao utazitatua kwa Muda mrefu” Alisema Prof. Mkumbo.
“MKUMBI II unalenga kuchambua mazingira ya biashara yaliyopo, mafanikio na changamoto zake, na kutoa mapendekezo yatakayokuwa suluhisho la muda mrefu” Alisema Prof. Mkumbo.
Mpango huu ni muhimu katika kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha juu cha kati, ikiwa na Pato la Taifa (GDP) la dola za Marekani trilioni moja na pato la mtu mmoja mmoja la dola 7,000.
Sekta binafsi inatarajiwa kuwa injini muhimu ya ujenzi wa uchumi huo, hivyo kuwepo kwa mazingira bora ya biashara na uwekezaji itakuwa hatua Madhubuti kuelekea utekelezaji wa Dira 2050.