Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

SEKTA BINAFSI INATARAJIWA KUCHANGIA SHILLINGI TRILIONI 60.1 (SAWA NA ASILIMIA 69.6), IKIWA NI GHARAMA ZA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2026/2027


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo (Mb) , amebainisha kuwa Sekta Binafsi inatarajiwa kuchangia shillingi Trilioni 60.1 (sawa na asilimia 69.6), ikiwa ni gharama za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2026/2027, huku gharama za utekelezaji wa Mpango huo zinakadiriwa kuwa TZS trilioni 86.3.

Prof. Mkumbo ameyasema hayo Bungeni alipokuwa akiwasilisha kwenye Mkutano wa Wabunge wote Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/27, Mkoani Dodoma.

Amefafanua kuwa mchango wa sekta binafsi unatarajiwa kupatikana kupitia uwekezaji katika ukuzaji mitaji, hususani katika mali za kudumu na shughuli za kiuchumi na kijamii kama vile viwanda na biashara, nishati na madini, kilimo, mifugo na uvuvi, maji, afya, elimu, utalii, mitambo, mashine, miundombinu ya uzalishaji, miundombinu ya usafiri na usafirishaji, na teknolojia.

“Hivyo basi, sote tutahitaji kubadilika na kubadili mitazamo yetu kwa kujielekeza katika kuheshimu sekta binafsi na kuweka mazingira sahihi ya kukua kwake”. Amesema Prof. Mkumbo.

Akielezea mchango wa Serikali katika mpango huo amesema kuwa Serikali inatarajiwa kuchangia TZS trilioni 20.7 (24%) kutoka katika bajeti kuu ya serikali, na TZS trilioni 5.5 (6%) kutokana na uwekezaji wa mashirika ya umma.

Kwa upande wa Mashirika ya Umma amebainisha kuwa yanatarajiwa kutekeleza programu na miradi itakayopunguza ruzuku kutoka serikalini na kupunguza hasara, kuanzisha bondi za makampuni (corporate bonds), asset monetisation, kuunganisha baadhi ya mashirika ya umma ili kuongeza ufanisi, na kuwezesha mashirika ya umma kuingia katika masoko ya hisa ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika kukuza mitaji. Aidha, mashirika ya umma yanatarajiwa kuwekeza katika sekta mbalimbali, zikiwemo za nishati, usafiri na usafirishaji, kilimo, afya, miliki, utalii, mawasiliano, madini, huduma, na uzalishaji viwandani.

“Moja ya eneo kubwa la utofauti la mpango huu ukilinganisha na mipango iliyopita ni kutambuliwa bayana kwa ushiriki na mchango wa sekta binafsi katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huu wa maendeleo”.Amesema Prof. Mkumbo.