Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

SEKTA BINAFSI NCHINI KUCHANGIA 70% YA PATO LA TAIFA LA DOLA ZA MAREKANI TRILIONI 1 IFIKAPO MWAKA 2050


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji anayeshugulikia Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa amesema mwelekeo wa Wizara katika eneo la Biashara na Uwekezaji, uwe ni kuifanya sekta binafsi kuwa bora zaidi katika kuchangia 70% ya Pato la Taifa la dola za Marekani Trilion moja ifikapo 2050.

Dkt. Msemwa amesema hayo wakati wa kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji uliofanyika jijini Dodoma.

Amesema hatua ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji yana lengo kubwa la kuongeza kwa ushiriki wa sekta binafsi na umma katika biashara.

“Kama Wizara tujue kuwa tuna kazi kubwa na muhimu sana ya kufanya katika kuchangia pamoja na mambo mengine kuchochea upatikanaji wa ajira kwa vijana wetu kupitia biashara na uwekezaji, “ alisema Dkt. Msemwa.

Dkt. Msemwa aliwambia watumishi hao, kuzingatia ubora wa kazi zao kama mfumo wa PEPMIS unavyowataka watumishi wote kuutumia kwa ajili ya kuleta matokeo chanya kwenye biashara na Uwelkezaji hapa nchini.

Aliongeza kuwa ataendeleza juhudii zilizokuwepo za kuwafanya watumishi kuwa na weledi mkubwa, maarifa na uzoefu ili kutoshindwa chochote kwa kutokuwa na maarifa kwa kuhakikisha wanapewa maarifa ndani na nje ya nchi.

“Tutafute kwa njia yoyote yakupata maarifa bila kusubiri mafunzo yaliyoandaliwa na Wizara kwani yale ya Wizara yatakuwepo lakini machache na ni ya muda mfupi. Hivyo basi, tujaribu tutumia vyanzo vingine vya kujifunza ili kila Jumatatu inayokuja iwe ya tofauti na nyingine kwa kusonga mbele kwenye maarifa,” alisema na kuongoza kuwa kutokana na unyeti wa masuala ya biashara na uwekezaji, bila kuwa na maarifa kuna uwezekano wa kuliletea Taifa hasara kubwa kutokana na kufanya majukumu bila kuwa na uelewa.