Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

TANZANIA NA URUSI KUFUNGUA FURSA MPYA ZA BIASHARA, KILIMO NA UWEKEZAJI


Tanzania na Urusi zimeendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kupitia makubaliano mapya yatakayofungua fursa katika sekta za biashara, kilimo, uwekezaji, viwanda pamoja na matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Urusi.

Makubaliano hayo yamejadiliwa katika Kikao cha Tatu cha Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Biashara na Uchumi kati ya Tanzania na Urusi kilichofanyika jijini Arusha, kikihusisha viongozi wa serikali, wawekezaji, wafanyabiashara na wadau wa maendeleo kutoka mataifa hayo mawili.

Akizungumza Mei 16, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema ushirikiano huo unalenga kuongeza biashara kati ya Tanzania na Urusi, kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali na kufungua masoko mapya ya mazao ya kilimo pamoja na bidhaa zinazozalishwa nchini.

Amesema Tanzania itanufaika kupitia uwekezaji katika viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, teknolojia ya uzalishaji, usafirishaji wa bidhaa pamoja na ushirikiano wa kibiashara utakaowaunganisha wafanyabiashara wa nchi hizo mbili.

Katika kikao hicho, pande hizo mbili pia zimekubaliana kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Urusi ili kurahisisha mahusiano ya biashara, utalii na ushirikiano wa kiuchumi, huku ikitajwa kuwa hatua muhimu katika kuitangaza Tanzania na Afrika Mashariki kimataifa.

Mkataba wa matumizi ya Kiswahili ulisainiwa kati ya Mtendaji Mkuu wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Bi. Consolata Mushi na Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Shirikisho la Urusi, Bw. Maxim Reshetnikov.

Aidha, Tanzania na Urusi zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta za viwanda, miundombinu ya usafirishaji, nishati pamoja na usafiri wa anga, ikiwemo mpango wa kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kati ya Tanzania na Urusi ili kurahisisha biashara, utalii na uwekezaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda amesema makubaliano hayo yataongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi na kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Urusi.