Habari
TANZANIA NA UN KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI NA UWEKEZAJI

Juni 09, 2025 Dar es Salaam.
Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano uliyopo na Umoja wa Mataifa (UN) hususani katika sekta za Uwekezaji na Uchumi.
Hatua hiyo imebaina leo jijini Dar es Salaam, wakati Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi M. Kida, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bi. Susan Ngongi Namondo, kuhusu masuala yanayohusu Uchumi na uwekezaji.
Katika mazungumzo yao, Dkt. Kida alimueleza Bi. Susan jinsi Tanzania inavyoendelea kujiimarisha katika kubainisha vipaumbele vya kitaifa kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
"Tunaweka mikakati thabiti kuhakikisha malengo yetu ya maendeleo yanatekelezwa kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta binafsi kwa kuangazia na kuhakikisha kuwa tunaweka mazingira mazuri ya ufanyaji biashara na uwekezaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuendelea kupanua wigo wa kuiwezesha sekta binafsi kupata mitaji kupitia majukwaa mbalimbali ya kifedha." Alisema Dkt. Kida.
Aidha, alieleza juhudi za serikali katika kuoanisha mipango ya Kitaifa na mikakati mbalimbali ya maendeleo ya Umoja wa Mataifa ili kufikia malengo ambayo tumejiwekea kama nchi.
Kwa upande wake, Bi. Susan alishukuru Tanzania kwa ushirikiano wake na UN, ambapo alieleza kufurahishwa na jitihada za Tanzania, ikiwemo namna ambavyo Tanzania imeendelea kuratibu na kufanya tathmini ya utekelezwaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Pamoja na mambo mengine, wawili hao walikubaliana kuendeleza ushirikiano katika utekelezaji wa Malengo Endelevu (SDGs).