Habari
TANZANIA NA URUSI KUIMARISHA USHIRIKIANO WA BIASHARA NA UWEKEZAJI
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Pius Stephen Chaya ameikaribisha Nchi ya Urusi kuwekeza Nchini Tanzania.
Dkt. Chaya ameyasema hayo leo tarehe 15 May, 2026 wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi ambapo ameeleza namna Tanzania inavyoendelea kujenga mazingira bora ya uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa.
Katika ufunguzi wa Jukwaa hilo, Dkt. Chaya amesema kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza mageuzi makubwa ya kiuchumi chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuifanya nchi kuwa kitovu cha biashara, viwanda na uwekezaji barani Afrika.
“Nawahimiza wawekezaji wa Urusi kutumia fursa zilizopo nchini Tanzania katika sekta ya madini, kilimo, viwanda, nishati, teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na elimu ya ufundi” Amesema Dkt. Chaya.
Dkt. Chaya ameongeza kuwa Tanzania inalenga kufikia uchumi wa kiwango cha juu ifikapo mwaka 2050 kupitia dira ya maendeleo inayoweka mkazo katika viwanda, ubunifu na ushiriki wa sekta binafsi. Alibainisha pia kuwa ushirikiano huu utaongeza biashara, ajira, uhamishaji wa teknolojia na maendeleo ya viwanda nchini.
“Matumaini makubwa kuhusu mustakabali wa ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi umeleta kampuni 120 za Urusi na mamia ya wafanyabiashara wa Tanzania ni ishara ya kuimarika kwa mahusiano ya kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili. Aliongeza Dkt. Chaya.
