Habari
2024 Mwaka wa Kitaifa wa Kuhamasisha Uwekezaji Nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa Serikali imeandaa kampeni maalum inayoendeshwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) iliyoanza Januari 8 na inatarajiwa kukamilika Februari 9, 2024 inayolenga kutoa elimu ya uwekezaji kwa wananchi ikiwemo kuondoa dhana kuwa ili kuwekeza nchini lazima uwe mgeni au uwe tajiri.
Ameyasema hayo leo Januari 11, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Mhe. Waziri Prof. Mkumbo ameeleza kuwa kupitia utekelezaji wa sera na sheria mbalimbali za uwekezaji na maelekezo mahususi ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kupata mafanikio mbalimbali katika kuhamasisha, kuvutia na kuwezesha uwekezaji nchini.
“Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji Uwekezaji ilizinduliwa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kwa lengo la kutoa msukumo maalum kwa Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo nchini”, amesema Mhe. Prof. Mkumbo.
Aidha, amefafanuwa kuwa katika utekelezaji wa kampeni hiyo Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, kupitia TIC, imeamua kuufanya mwaka 2024 kuwa mwaka wa kitaifa wa kuhamasisha uwekezaji nchini.
Mhe. Prof. Mkumbo amebainisha kuwa kupitia kampeni hiyo kutakuwa na fursa ya kueleza taratibu za kusajili miradi ya uwekezaji kupitia TIC, kueleza vivutio mbalimbali vya kikodi na visivyo vya kikodi vinavyotolewa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wanaposajili miradi yao na kuonesha mafanikio na fursa ambazo Watanzania wamepata katika uwekezaji kupitia TIC.
Fursa zingine za kampeni hiyo ni pamoja na kusikiliza, kupokea na kutatua changamoto zinawakabili Watanzania katika uwekezaji na mazingira ya biashara kwa ujumla, kukuza ushirikiano na waandishi wa habari katika kuongeza wigo wa uelewa kuhusu dhana na taratibu za uwekezaji nchini na kukuza ushirikiano na Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na viongozi wa sekta binafsi katika mikoa na wilaya.
Aidha, kupitia utekelezaji wa sera na sheria mbalimbali za uwekezaji nchini zaidi ya ajira 230,000 zinatarajiwa kuzalishwa kufuatia TIC kusajili miradi 504 yenye thamani ya dola za kimarekani 56 bilioni katika kipindi cha mwaka 2023.