Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

MAWAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO AFRIKA WATUPIA JICHO MATUMIZI YA AKILI MNEMBA


Mkutano wa 56 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Kiuchumi umehitimishwa jana nchini Zimbabwe huku mawaziri wa hao wakikubaliana masuala mbalimbali ikiwemo Nchi wanachama kuweka mazingira wezeshi kuhusu matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence) kama nyenzo muhimu katika ulimwengu wa kidijitali.

Kwa mujibu wa mjadala katika mkutano huo, msisitizo wa kuweka mazingira wezeshi ya matumizi ya akili mnemba yatachochea maendeleo ya kiuchumi.

Maeneo mengine yaliyoangaziwa kwa kina na kufikia makubalino ni kuendeleza ushirikiano wa kikanda ikiwa ni pamoja na kuibua miradi itakayounganisha na kuleta manufaa kwa nchi wanachama.

Vilevile, mawaziri hao wamekubaliana kupaza sauti kuhusiana na vikwazo ambavyo vimekuwa vikiwekwa kwa baadhi ya nchi na kuzisababishia mazingira magumu kufikia malengo ambayo Afrika imejiwekea.

Mkutano wa 57 wa Mawaziri hao unatarajiwa kufanyika nchini Ethiopia na utabeba kaulimbiu isemayo "Kuibua mikakati mahsusi itakayowezesha Afrika kutekeleza masuala yaliyobainishwa kwenye mkataba wa uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Katika mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, aliwakilishwa na Katibu Mkuu wake Dkt. Tausi Kida.