Habari
DIRA 2050 KUZINDULIWA TAREHE 17 JULAI, 2025 - PROF. MKUMBO

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza kukamilika kwa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, baada ya mchakato wa zaidi ya miaka miwili. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alisema hayo Julai 8, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati akieleza hatua zilizofikiwa kuelekea uzinduzi rasmi wa Dira hiyo.
Mchakato ulianza Februari-Machi 2023 kwa maandalizi ya miongozo ya uandishi na kuzinduliwa rasmi Aprili 3, 2023 na Makamu wa Rais kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan. Hatua zilizokamilika ni pamoja na kuunda vyombo vya kusimamia mchakato, kufanya tathmini ya Dira ya 2025, kukusanya maoni ya zaidi ya watu milioni moja, kufanya ziara za kujifunza nje ya nchi, na kuandaa rasimu mbili.
Rasimu ya Pili iliwasilishwa kwa Waziri Mkuu, kisha kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri na kuridhiwa na Bunge tarehe 22 Juni 2025, hatua iliyowezesha Dira kupata uhalali wa kitaifa na ulinzi wa kikatiba. Prof. Mkumbo amesema Serikali sasa inajiandaa kwa uzinduzi rasmi wa Dira hiyo tarehe 17 Julai 2025 mjini Dodoma, utakaofanywa na Rais Samia, aliyehimiza uwepo wa dira itakayoongoza maendeleo jumuishi, ya viwanda na TEHAMA ifikapo 2050.