Habari
DKT. KIDA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI WA MAENDELEO WA OFISI YA UBALOZI WA UINGEREZA NCHINI TANZANIA
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida alikutana na kufanya mazungumzo na Bi. Anna Wilson, Mkurugenzi wa Maendeleo wa Ofisi ya Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania Septemba mosi jijini Dar es Salam.
Katika Mazungumzo yao, viongozi hao walijadiliana namna ya kuimarisha ushirikiano katika uandaaji na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kiuchumi hususani kukuza uwekezaji wa sekta binafsi na sekta ya umma.
Ushirikiano wa kibiashara, kukuza uwekezaji, Malengo ya Ushirikiano wa Ufanisi wa Pamoja, Ushirikiano katika utekelezaji wa malengo ya Dira 2050, pamoja na mapitio ya Mpango wa Ushirikiano wa Maendeleo (MPP) uliosaini wa Aprili 2024, vilitawala mazungumzo ya viongozi hao.
Kuhusu MPP, pamoja na mambo mengine, walijadili utekelezaji wa Mpango huo uliyopata mafanikio katika kuvutia miradi ya uwekezaji 51 kutoka nchi ya Uingereza inayotarajiwa kuwekeza kiasi cha paundi za Uingereza milioni550.47 katika kipindi cha mwaka mmoja, ukilinganisha na kiasi cha miradi 979 yenye mtaji wa paundi 4,223.34 milioni iliyosajiliwa katika kipindi cha mwaka 1997 hadi Aprili, 2024.
Itakumbukwa kuwa, malengo ya Mpango huo ilikuwa ni kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi kufikia paundi za Uingereza 300 milioni kwa mwaka.
Aidha, Katibu Mkuu Dkt. Kida na Mgeni wake waliangazia namna ya kukuza biashara kwa kiwango cha paundi za Uingereza 100 milioni na kuvutia uwekezaji kutoka taasisi za uwekezaji za Serikali ya Uingereza kiasi cha paundi 1 bilioni.
Kuhusu Dira 2050 iliyozinduliwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Julai 17 mwaka huu, Dkt. Kida hakusita kueleza matarajio yake kwa Serikali ya Uingereza kuendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo katika utekelezaji wa malengo ya Dira hiyo ya kukuza Uchumi wa Taifa kufikia dola za Marekani trilioni 1 huku kipato cha mtu mmoja kikitarajiwa kufikia dola 7,000.
Dkt. Kida alitumia fursa hiyo kumkaribisha Bi. Anna aliyefika kwa ajili ya kujitambulisha katika nafasi yake hiyo mpya nchini.
Kwa upande wake, Bi. Anna Wilson, alipongeza jitihada za Serikali ya Tanzania katika kukuza uchumi na kuboresha mazingira ya biashara na alieleza kwamba ana matumaini makubwa kwa Tanzania kufikia malengo ya Dira 2050.
