Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

DKT. KIDA AWAHAKIKISHIA WAWEKEZAJI KUTOKA AUSTRIA MAZINGIRA MAZURI YA UWEKEZAJI.


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejidhatiti katika kuboresha mazingira ya Uwekezaji kwa kufanya mapitio ya Sera, Sheria na Mifumo ya uwekezaji na biashara nchini.

 

Vilevile, amewakaribisha wawekezaji kutoka Austria kuja kuwekeza nchini na kutumia fursa zinazotokana na mazingira mazuri ya uwekezaji Tanzania.

 

Ameyasema hayo Oktoba 25, 2023 jijini Dar es Salaam alipokutana na ujumbe wa Serikali na Wawekezaji kutoka nchini Austria ulioongozwa na Waziri wa Kazi na Uchumi wanchi hiyo Mhe. Prof. Dkt. Martin Kocher, wakati ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii.  Mhe. Angela Kairuki (Mb).

 

Dkt. Kida ameeleza kuwa maboresho yaliyofanyika nchini yamewezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazovutia kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji akirejea tafiti na ripoti zinazotolewa na taasisi za kimataifa zikiwemo UNCTAD na KPMG.

 

Alisema nchi ya Austria na Tanzania zina ushirikiano wa muda mrefu ambao umewezesha kupatikana kwa mafanikio katika sekta mbalimbali akitolea mfano miradi iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) yenye thamani ya dola za Marekani Milioni 35.27.

 

Naye Waziri wa Kazi na Uchumi wa Austria Mhe. Prof. Dkt. Martin Kocher ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa inayopiga katika kukuza uchumi na kuvutia uwekezaji.Alieleza kuwa ujumbe wa wawekezaji alioambatana nao umevutiwa na wameonyesha nia ya kuwekeza Tanzania.

 

Aliongeza kuwa ujumbe huo umejumuisha wawekezaji kutoka sekta za afya, ufundi na ujuzi, nishati, utalii na TEHAMA.