Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

DKT. MPANGO AFUNGA KONGAMANO LA UWEKEZAJI TANZANIA - CHINA AKITAMANI KUKUA KWA BIASHARA


Makamu wa Rais, Mhe. Dkt philip Mpango amesema anatamani kuona kiwango cha biashara baina ya Tanzania na China kinaongezeka.  

Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo leo Machi 27, 2024 alipofunga Kongamano la Uwekezaji baina ya wawekezaji wa Tanzania na China jijini Dar es Salaam akisema kuwa Tanzania imewekeza kwenye miundombinu wezeshi ya uwekezaji ikiwemo ujenzi wa Reli (SGR), Bwawa la kuzalisha umeme (JNHP), Upanuzi na uendeshaji wa kisasa wa Bandari ya Dar es Salaam. 

"Hadi kufikia January 2024 China wameweza kusajili miradi Tanzania 1,274 yenye thamani ya kiasi cha dola za Marekani 11,402.08 milioni inayotarajia kuzalisha ajira zipatazo 149,759" Alisema Dkt. Mpango. 

Kongamano hilo lilowakutanisha wawekezaji na wafanyabiashara zaidi ya 250 wa ndani ya nchi na 60 kutoka China, limeshuhudia utiaji saini wa Makubaliano ya Mashirikiano (MoUs) katika miradi 4 ya sekta za uchumi na biashara, kilimo na ujenzi. 

Aidha, Dkt. Mpango ametumia jukwaa hilo kutoa rai kwa wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo wa China kuongeza uwekezaji kwenye miradi inayozingatia mabadiliko ya tabia nchi (green grow) ili kusaidia juhudia za Tanzania katika mageuzi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na miradi ya uchumi wa blue

Awali, akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, alisema kuwa ajenda ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasa ni kuona sekta binafsi inakua na kwamba sekta hiyo inapiga hatua kwa sababu ya msukumo na uungwaji mkono wa Rais. 

"Septemba 2023, tulikuwa na Kongamano kama hili ambapo karibu wawekezaji mia 100 kutoka China walifika na tunaona mwaka huu wengi wamewekeza kwenye Kongani ya viwanda ya Kwala Kibaha ambako utekelezaji wa ujenzi wa viwanda 200 unaendelea" Alisema Prof. Mkumbo.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chen Mingjian amesema kuwa, kampuni za China zinaiona Tanzania Kama kitovu cha uzalishaji na shabaha yao ni kuuza bidhaa wanazozalisha nchini katika masoko ya nchi za Afrika hatua ambayo inaisaidia Tanzania kupata fedha za kigeni. 

Uhusiano wa Tanzania na China umedumu tangu ulipoasisiwa mwanzoni mwa miaka ya 60 na waasisi wa mataifa haya mawili Mwalimu Julius K. Nyerere wa Tanzania na Mao Zedong wa China na uwekezaji wa Reli ya Tazara kati ya Tanzania na Zambia ukiwa unabaki kuwa alama ya historia ya ubia wa biashara na uwekezaji baina ya mataifa haya mawili.