Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

MHE. DKT. SAMIA AKUTANA NA MAKAMU WA RAIS WA BENKI YA UWEKEZAJI YA ULAYA (EIB), BW. THOMAS OSTROS


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) Bw. Thomas Östros wamekutana na kujadili ushirikiano, ikijumuisha uwekezaji katika sekta ya Umma na Binafsi. 

Pamoja na mambo mengine, wawili hao wamejadiliana kuhusu maendeleo ya miradi inayofadhiliwa na EIB nchini, ambapo Bw. Östros, alimueleza Mheshimiwa Rais jinsi wanavyoridhishwa na usimamizi wa miradi yao hapa Tanzania.

Aidha, Bw. Östros, alieleza kuwa EIB ina mpango wa kuendeleza mashirikiano na Benki za kitanzania ili kuunga mkono sekta mbili za kipaumbele ambazo ni jinsia (gender) na uchumi wa Buluu.

Mheshimiwa Rais, alimshukuru Bw. Östros kwa msaada unaotolewa na EIB nchini akivutiwa na nia ya EIB kuendelea kuunga mkono Uchumi wa Buluu hususani kutoa ruzuku kwa wanawake wajasiriamali wanaojishughulisha na kilimo cha Mwani huko Zanzibar.

Vile vile, Mhe. Rais alieleza umuhimu wa msaada kutoka EIB utakaosaidia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza aikiutazama Mkoa huo kama kituo muhimu cha biashara kama ilivyo Dar es Salaam.

Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) ni miongoni mwa wadau muhimu wa Maendeleo wa Tanzania kwa muda mrefu.