Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

MHE. KIKWETE AWATAKA WATUMISHI WA OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI KUZINGATIA MAFUNZO YA PEPMIS NA PIPMIS.


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb,) amewataka watumishi wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kuzingatia mafunzo wanayopewa ili kuboresha utendaji kazi wa watumishi na taasisi kwa ujumla.

Mhe. Kikwete ameyasema hayo leo tarehe 19 Desemba, 2023 jijini Dodoma alipofungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kupima utendaji kazi wa mtumishi na taasisi ya PEPMIS na PIPMIS.

Mhe. Kikwete ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan inalenga kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi ndio maana menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora kuja na mfumo huu unaolenga kutatua changamoto za upimaji utendaji wa watumishi, kujua mwelekeo wa taasisi kiutendaji katika kuwahudumia wananchi.

“Nawapongeza sana waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb,) pamoja na Katibu Mkuu Dkt. Tausi Kida kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya katika kuitengeza Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na hasa kupitia kazi ya ukusanyaji maoni kwa ajili ya uandaaji wa Dira ya taifa ya 2050 ambayo itaenda kuonesha mwelekeo wa Nchi kwa miaka 25 ijayo” Amesema Mhe. Kikwete.

Aidha, Katibu Mkuu Dkt. Tausi Kida amesema kuwa majukumu ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ni pamoja na kusimamia tume ya mipango, Ofisi ya msajili wa hazina yenye mashirika zaidi ya 300, kusimamia sekta binafsi katika masuala ya sera na sheria katika uwekezaji kupitia Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) na Mamlaka ya eneo huru la uwekezaji (EPZ).

“Tunaishukuru sana Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora kwa kuja na mfumo huu kwani utasimamia ufanisi wa kiutendaji na kuleta haki kwa watumishi wa umma, sisi tumeufurahia mfumo huu ambao utaenda kuongeza tija katika kuwahudumia wananchi na kuboresha maeneo ambayo yatakuwa na changamoto kuongeza ufanisi” Amesema Dkt. Kida.