Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb,) amesema kuwa Mwaka 2023, Pato halisi la Taifa lilifikia shilingi trilioni 148.3 kutoka shilingi trilioni 141.2 mwaka 2022, sawa na ukuaji wa asilimia 5.1 ikilinganishwa na asimilia 4.7 mwaka 2022. Ukuaji huo ulichangiwa na jitihada mbalimbali za Serikali ikiwemo: mikakati ya kukabiliana na athari za vita kati ya Ukraine na Urusi pamoja na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu na usafirishaji; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini, hususan dhahabu na makaa ya mawe; na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi iliyochachua shughuli za kiuchumi.
Mhe. Prof. Mkumbo ameyasema hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi kwa mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/2025 katika Bunge la 12 mkutano wa 15, kikao cha 47 bungeni, jijini Dodoma.
Mhe. Prof. Mkumbo ameongeza kuwa mwaka 2023, sekta ya sanaa na burudani iliongoza kwa kuwa na ukuaji wa asilimia 17.7 ikifuatiwa na sekta ya fedha na bima asilimia 12.2, madini asilimia 11.3, malazi na huduma za chakula asilimia 8.3, na habari na mawasiliano asilimia 7.6. Aidha, shughuli ya kilimo iliongoza kwa kuwa na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa kwa asilimia 26.5 ikifuatiwa na ujenzi asilimia 13.2, madini asilimia 9.0 na biashara na matengenezo asilimia 8.3.
“Tathmini ya muda mrefu ya uchumi wa Tanzania inaonesha uchumi umekuwa stahimilivu na kukua katika hali endelevu licha ya changamoto zilizoyumbisha uchumi wa dunia katika vipindi mbalimbali, ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi, ugonjwa wa UVIKO – 19, na vita mbalimbali pia kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi” Amesema Mhe. Prof. Mkumbo.
Aidha Prof. Mkumbo amepongeza juhudi za rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuliongoza Taifa letu kwa weledi, umahiri na utulivu mkubwa katika kipindi chake cha miaka mitatu ambapo ameonesha weledi na kuthibitisha uadilifu na uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yetu.
Mhe. Mkumbo ameongeza kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia amejenga maridhiano mapana ya kijamii na kisiasa na kuweka mazingira sawia ya kufanya siasa kwa vyama vyote nchini, ametoa uhuru wa kutosha wa kutoa maoni bila woga wala vitisho na kuleta mageuzi makubwa katika mazingira bora ya biashara na uwekezaji kwa kuimarisha sekta za kilimo, mifugo, uvuvi na madini.
ameeleza kuwa programu na miradi 193 ikiwemo miradi ya kielelezo 17 inatekelezwa katika kufikia malengo ya mpango wa miaka mitano kwa kuzingatia vipaumbele mbalimbali ikiwemo Ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge Railway – SGR), Mradi wa uboreshaji Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ambapo ndege mbili aina ya Boeing 737-9 Max zimepokelewa na kufanya ndege zinazomilikiwa na ATCL kufikia 16.
Mhe. Prof Mkumbo ameeleza vipaumbele kumi vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/2025 iikiwa ni Kuendelea kulinda mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano iliyopita, Kuendelea na juhudi za kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula nchini kwa kuendelea kuongeza matumizi ya mbolea, mbegu bora na kilimo cha umwagiliaji, Kuongeza uzalishaji na uuzaji wa bidhaa (pamoja na huduma) nje ya nchi kupitia sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, misitu na madini, Kuweka mkazo wa pekee katika kuongeza thamani katika mazao yanayozalishwa kupitia sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, misitu na madini, Kuendelea kuongeza, kuboresha na kuimarisha ubora wa huduma za jamii, ikiwa ni pamoja na elimu, afya, maji na umeme.
Mhe. Prof. Mkumbo ameongeza vipaumbele vingine ni pamoja na Kuendelea kupanua na kuimarisha miundombinu ya usafiri wa barabara, reli, anga, majini na utunzaji endelevu wa mazingira, Kujielekeza kwenye kufungua fursa katika sekta za madini ya kimkakati (critical minerals), uvuvi wa bahari kuu (deep sea fishing), uchumi wa kijani (green economy) na uchumi wa kidigitali (digital economy), Kuendelea kuchukua hatua stahiki katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, ikiwemo kuetekeleza mkakati wa miaka kumi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na Kukamilisha maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.