Habari
PROF. MKUMBO AIPONGEZA DSE NA NMB KWA KUJA NA MFUMO WA HISA KIGANJANI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo ameipongeza Benki ya NMB kwa kushirikiana na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kuzindua mfumo wa DSE Hisa Kiganjani kupitia aplikesheni ya NMB Mkononi.
Mhe. Mkumbo ameyasema hayo leo tarehe 10 Julai, 2025 jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa DSE Hisa Kiganjani kupitia aplikesheni ya NMB Mkononi.
Prof. Mkumbo ameongeza kuwa hatua hii inaonesha namna teknolojia inavyoweza kuwa kichocheo cha uwekezaji kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma, kuokoa muda na kupunguza gharama.
“Takwimu zinaonesha kuwa tangu Januari 2023 hadi Julai 2025, thamani ya ununuzi na uuzaji wa hisa imefikia shilingi bilioni 756.42, huku biashara ya kidigitali kupitia Hisa Kiganjani ikichangia shilingi bilioni 45.56. Jumla ya wawekezaji wapya 81,000 wamejiunga na mfumo huu wa kidigitali, na matarajio ni kuvuka idadi ya wawekezaji milioni moja kwa mwaka, jambo linaloashiria mwamko mpya wa uwekezaji nchini. Amesema Prof. Mkumbo.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi. Ruth Zaipuna amesema kuwa kupitia ushirikiano huu kati ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kupitia aplikesheni ya NMB Mkononi utawawezesha wateja wa NMB kujisajili, kununua na kuuza hisa, kupata taarifa ya thamani ya uwekezaji wao kwa wakati halisi, kuona bei za hisa za makampuni yote yaliyoorodheshwa katika soko la hisa la Dar es salaam.
“Mfumo huu unalenga kurahisisha huduma wa ununuzi na uuzaji wa hisa kwa kuwafikia wananchi popote walipo kupitia simu zao za mkononi. Amesema Bi. Zaipuna.
Vilevile, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE) Bw. Peter Situmbeko Nalitolela amesema kuwa tukio hili linaashhiria hatua kubwa ya kimaendeleo katika sekta ya masoko ya mitaji, siyo tu kwa DSE na NMB bali kwa taifa zima.
Bw. Nalitolela ameongeza kuwa uzinduzi wa Hisa kiganjani kupitia aplikesheni ya NMB kiganjani ni jambo kubwa sana katika kuhakikisha uwekezaji unafikika kwa kila mtanzania, uelewa wa masoko ya mitaji unaongezeka na ujumuishaji wa kifedha unakuwa wa kweli na siyo nadharia.