Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

MHE. PROF. MKUMBO ASHIRIKI JUKWAA LA GLOBAL GATEWAY NCHINI UBELGIJI.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb), amemwakilisha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Global Gateway Forum uliofanyika tarehe 25 na 26 Oktoba 2023, Brussels, Ubelgiji.
 
Global Gateway Investment Package ni mpango wa EU wa kuchochea uwekezaji duniani hususan barani Afrika ambako Mpango huo unalenga kuchochea uwekezaji wa jumla ya Euro billioni 150 barani Afrika.
 
Mhe. Mkumbo ameshiriki katika maeneo makubwa matatu ikiwemo kushuhudia utiaji saini wa mkataba baina ya EU na Shirika la Maendeleo la Ufaransa
(AFD) ambapo EU imetoa msaada kwa Tanzania wa Euro milioni 36 sawa na Shilingi bilioni 95 kwa ajili ya Mradi wa uzalishaji wa umeme kwa njia yamaji wa Kakono, Mkoani Kagera (MW 87.8), Mradi huo wenye jumla ya euro million 288.11 sawa na takribani shilingi bilioni 800 unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kupitia mikopo nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na msaada wa EU. 
 
Mheshimiwa Mkumbo ameishukuru EU kwa msaada wake kwenye Mradi huo na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania itasimamia kikamilifu utekelezaji
wake. Mhe. Prof. Mkumbo ameshiriki na kuchangia kwenye mijadala yenye lengo la kuweka mikakati ya pamoja kwenye masuala ya madini ya kimkakati na mageuzi ya kidijtali. Kwa upande wa madini ya kimkakati, majadiliano na makubaliano yamefikiwa kwamba Mpango wa Global Gateway uchochee uwekezaji unaowezesha madini ya kimkakati kuongezewa thamani katika nchi yanakochimbwa badala ya thamani kuongezwa baada ya madini hayo kuuzwa nje.
 
Mhe. Prof. Mkumbo ameuhakikishia mkutano huo utayari wa Serikali ya Awamu ya Sita kupokea uwekezaji huo na tayari mazingira 
mazuri na rafiki ya uwekezaji yamewekwa. Kwa upande wa mageuzi ya kidijitali Tanzania imeshiriki kwenye majadiliano na hatimaye makubaliano kufikiwa kwa mpango huo kuongeza kasi ya uwekezaji katika maeneo yanayochochea maendeleo ya kidijitali katika kilimo, elimu, biashara, afya na mengineyo na kuhimiza mageuzi ya kidijitali yachochee zaidi maendeleo ya wananchi wakiwemo wa vijijini.