Habari
MHE. PROF. MKUMBO ATOA MWONGOZO WA KUANDAA MKAKATI WA KITAIFA WA UHAMASISHAJI UWEKEZAJI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji (OR-MU), Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb), ameongoza mkutano maalumu na timu ya wataalamu wanaoandaa Mkakati Unganishi wa Kitaifa wa Kuimarisha Shughuli za Uhamasishaji Uwekezaji (NIPS).
Mkutano huo ulifanyika jijini Dodoma, ukiwa na lengo la kuweka mwelekeo wa kitaifa wa kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kipindi cha zaidi ya miaka kumi.
Akitoa maelekezo kwa timu ya wataalamu, Mhe. Prof. Mkumbo alieleza kuwa mkakati huo utakuwa nyenzo muhimu katika kuongeza tija kwenye sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji nchini.
“Serikali inatambua umuhimu wa uwekezaji wa ndani na nje katika sekta mbalimbali katika kuzalisha ajira, kuboresha ubunifu, na kurahisisha uhawilishaji wa teknolojia, jambo ambalo litasaidia ukuaji wa uchumi endelevu,” alisema.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Sekta Binafsi wa OR-MU, Bw. Aristides Mbwasi, alieleza kuhusu mchakato wa awali wa utekelezaji wa kuandaa mkakati huo uliyohusisha kuandaa hadidu za rejea na aligusia ushiriki wa wadau mbalimbali wakiwemo Trade Mark Afrika (TMA) na DAIMA associates.
Bw. Mbwasi alisema kuwa, hadi sasa Mshauri mwelekezi ambaye ni DAIMA Associates anaendelea kushirikiana na Wataalamu wa OR-MU na wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi kuhakikisha mkakati unaoandaliwa unakidhi mahitaji ya nchi na kuongeza tija katika uwekezaji.
Kwa upande wake, Prof. Samuel Wangwe, ambaye ni Mshauri Elekezi, aliipongeza Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa juhudi zake katika kuhamasisha uwekezaji, akisisitiza kuwa mkakati unaoandaliwa utabainisha sekta za kipaumbele na changamoto zinazokwamisha uwekezaji.
Serikali ya awamu ya sita inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa kutengeneza fursa zaidi za kiuchumi na hatua ya kuandaa Mkakati Unganishi wa Kitaifa wa Kuimarisha Uhamasishaji wa Uwekezaji ni moja kati ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali, na Mkakati huo unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta ya uwekezaji, sambamba na kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje.