Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

MHE. PROF. MKUMBO ATOA WITO KWA WAKUU WA TAASISI: "MIELEKEO YA SERIKALI IWE MSINGI WENU"


Kibaha - Pwani, Oktoba 9, 2024 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb), ametoa wito kwa Wakuu wa Taasisi za Serikali, akiwataka kuzijua kwa undani taasisi wanazosimamia na kuelewa vipaumbele vya Serikali. 


Prof. Mkumbo ametoa wito huo wakati akizungumza na Wakuu wa Taasisi 111 walioteuliwa tangu mwaka 2022, katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha-Pwani.


Katika hotuba yake, Prof. Mkumbo alifichua ajenda muhimu zinazotarajiwa kupamba Dira ya Maendeleo 2050, akisema Serikali inalenga kujenga uchumi shirikishi, kupunguza umasikini, na taifa lenye kujitegemea na kustawi. "Viwanda vya kuongeza thamani vitakuwa kiini cha maendeleo yetu. Tunahitaji kuzalisha bidhaa zenye thamani badala ya kuendelea kuuza malighafi nje. Hii itahitaji miundombinu thabiti, hususan katika sekta ya nishati," amesema kwa msisitizo.


Prof. Mkumbo ameeleza kuwa, kuwekeza katika uzalishaji wa nishati na miundombinu kutaongeza uwezo wa nchi kujiimarisha katika masoko ya kimataifa kwa kuuza bidhaa badala ya malighafi. 


Ameongeza kuwa ni muhimu kwa Wakuu wa Taasisi kuwa na taarifa sahihi na za sasa kuhusu sekta wanazoziongoza, ndani na nje ya nchi, ili kuendana na mwelekeo wa taifa. "Ushahidi wa kitafiti na data sahihi ni silaha yenu. Fahamuni kuwa ninyi ni sura za taasisi zenu, na jamii haiwezi kutenganisha mamlaka yenu na nyinyi binafsi," amewakumbusha.


Mafunzo haya elekezi yalianza Oktoba 7 na yanatarajiwa kumalizika Oktoba 10, 2024, yakilenga kuwaandaa Wakuu hao wa Taasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali kwa majukumu yao ya uongozi, ili waweze kuchangia kwa ufanisi katika safari ya Tanzania kuelekea kwenye uchumi imara na shirikishi.