Habari
MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA MBIONI KUANZA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa Serikali inakaribia kukamirisha mazungumzo na muwekezaji ili kutekeleza mradi wa kimkakati wa Makaa ya mawe na chuma wa Liganga na Mchuchuma.
Prof. Mkumbo, ametoa kauli hiyo Septemba 24, 2025 jijini Dar es Salam alipozungumza na Wahariri wa vyombo vya habari kuhusu maendeleo ya maandalizi ya utekelezaji wa Dira 2050 iliyozinduliwa na Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan Julai 17, 2025.
"Mwaka 2015 utekelezaji wa mradi ulisitishwa kufuatia Serikali kubaini baadhi ya masharti ya Mkataba wa Ubia kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya Sichuan Hongda Corporation (SHG) hayakuzingatia kikamilifu maslahi ya nchi na katika kukwamua mradi huu mwaka 2017 Serikali iliunda timu maalumu ya majadiliano (Special Presidential Government Negotiation Team)” Alisema Prof. Mkumbo.
Pamoja na mazungumzo hayo, hadi mwaka 2020 hapakuwa na mwafaka baina ya Serikali na muwekezaji (SHG) ambaye aliuza mali zake kwa Kampuni ya SDIG mwaka 2024 inayomilikiwa na Serikali ya Jimbo la Sichuan-China, Kampuni inayokamilisha mazungumzo ya kimkataba na Serikali.
Kukamilika kwa mazungumzo, kutaondosha mkwamo wa muda mrefu na kuruhusu utekelezaji wa mradi huo wenye umuhimu mkubwa kwa uchumi wa nchi.
“utekelezaji wa mradi huu utaifanya Tanzania kuwa mzalishaji wa nne wa chuma baarani Afirka, makaa ya mawe yatazalisha umeme takribani megawati 600, kuna chuma kitakachozalisha malighafi za viwandani na sekta ya ujenzi, vile vile kuna madini ya titanium” Alisema Prof. Mkumbo.
Faida nyingine za utekelezaji ni kuzalisha ajira kuanzia ujenzi wa miundombinu hadi kwenye viwanda, kukuza uchumi na mzunguko wa fedha kwenye eneo la Liganga na Mchuchuma kutokana na ongezeko la watu na mahitaji.
Baadhi ya hoja za Serikali katika mazungumzo ilikuwa ni pamoja na Chuma kuchenjuliwa ndani ya nchi, ikiwa ni utekelezaji wa Dira 2050, pamoja Serikali iongeze share zake katika umiliki wa mradi huo.
Katika mkutano huo, Wahariri waliohudhuria akiwemo Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri ndugu Deodatus Balile walihoji na kupewa ufafanuzi kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu Mipango ya Kitaifa, Uwekezaji na Maboresho ya mazingira ya ufanyaji wa biashara na uwekezaji.