Habari
OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI, YAJIVUNIA ONGEZEKO LA UWEKEZAJI, AJIRA NA MITAJI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb), amesema kuwa ndani ya miaka mitatu ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kumekuwa na ongezeko la uwekezaji, ajira na kiwango cha mitaji nchini.
Akizindua Baraza la kwanza la wafanyakazi wa Ofisi hiyo leo, Machi 22, Prof. Mkumbo amesema Sera na Maono ya Mhe. Rais vimechochea kusajiliwa kwa miradi 1,075 ikilinganishwa na miradi 700 iliyosajiliwa miaka mitatu kabla ya uongozi wake.
"Katika uongozi wake Mhe. Rais ametengeneza ajira 137,000 kupitia uwekezaji ikilinganishwa na ajira 80,000 zilizotengenezwa miaka mitatu kabla yake, huku mitaji ikikua kwa dola za Marekani bilioni 14.2 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 6.1 miaka mitatu kabla yake " alisema Prof. Mkumbo.
Aidha, katika sekta ya Mipango na Uwekezaji Mhe. Rais Samia amekuwa ni Rais wa pili kupata fursa ya kuandika Dira ya Taifa tangu nchi ipate uhuru.
Kuhusu baraza hilo, Prof. Mkumbo amewaasa wafanyakazi kujiepusha na utamaduni wa kuogopa viongozi kwa kuwa unahatarisha utendaji wa taasisi.
"Kiongozi anapaswa kuheshimiwa sio kuogopwa, mimi sipendi kuogopwa na hii sekta yetu inahitaji tupate maarifa zaidi na tuendeleze utamaduni wa kujifunza."Alisema.
Vile vile, Prof. Mkumbo amewaasa wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kuepuka kuwasaidia viongozi kuvunja sheria.
"kuna watendaji wapo tayari kutekeleza maelekezo ya kiongozi bila kuangalia kama yanavunja sheria, mpe ukweli wa kisheria kiongozi wako akivunja atakuwa ameamua yeye, mkifanya hivyo mtatusaidia kutekeleza majukumu yetu kwa mujibu wa sheria,"alisema.
Pamoja na hayo, aliwaasa watumishi hao kuepuka tamaa katika maisha ya utumishi wa umma hasa tabia ya kutafuta vyeo kwa nguvu badala yake waache vyeo viwafuate.
"Hii tabia ya kutafuta vyeo inasababisha watu kutengenezeana ajali kazini , nina waasa sana fanyeni kazi zenu kwa weledi vyeo vitawafuata "alisema.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk.Tausi Kida, alisema baraza hilo ni muhimu katika kusimamia maslahi ya wafanyakazi na kushauri wafanyakazi kubuni Sera zitakazowavutia wawekezaji na kuboresha mazingira ya Biashara nchini.