Habari
PROF. MKUMBO ATAJA VIPAUMBELE 9 VYA OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Profesa Kitila Mkumbo (Mb.), amewasilisha bajeti ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na taasisi zilizo chini yake huku akiainisha vipaumbele tisa vitakavyotekelezwa katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Akiwasilisha hotuba hiyo Mhe. Prof Mkumbo alisema kuwa itakuwa ni pamoja na kuandaa Mpango wa Pili wa kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II).
Aidha, Ofisi hiyo itaendelea kuratibu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwa kuzingatia Dira Mpya ya Maendeleo ya Mwaka 2050 na Mpango wa Maendeleo wa Mwaka kwa mujibu wa Mwongozo wa Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2050.
Profesa Mkumbo ametaja vipaumbele hivyo leo Bungeni wakati akisoma Makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/2026 ambapo amesema katika mwaka ujao wa fedha Ofisi hiyo itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
“Ofisi imepanga kukamilisha mchakato wa kuunganisha taasisi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kusimamia Uzalishaji wa Bidhaa kwa Ajili ya Mauzo Nje ya Nchi (EPZA) kisha kuunda taasisi ya TISEZA ikiwa sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya kiuchumi ya mwaka 2025,”alisema Prof. Mkumbo.
Pia amesema Ofisi yake imepanga kuratibu ushiriki wa nchi na kusimamia majadiliano ya mikataba ya kimataifa ya uwekezaji katika ngazi ya kikanda na kimataifa, kuratibu na kusimamia uwekezaji katika kanda maalum za kiuchumi na kongani za viwanda.
Vile vile, Profesa Mkumbo ametaja mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa bajeti ya 2024/2025,ambapo alisema katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu, TIC ilisajili miradi mipya 691 yenye thamani ya dola milioni 7,997.06 ambayo ilitarajiwa kuzalisha ajira mpya 298,257.
Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 35.8 ukilinganisha na miradi 509 iliyosajiliwa mwaka 2023/24 ikiwa na thamani ya dola milioni 5,825.00 iliyotarajiwa kuzalisha ajira mpya 130,202.
Alieleza kuwa kati ya miradi 681 iliyosajiliwa kwa mwaka 2024/2025, asilimia 32 inamilikiwa na Watanzania pekee, asilimia 23 inamilikuwa kwa ubia katika ya Watanzania na wageni huku asilimia 45 ya miradi inamilikiwa na wawekezaji wa kigeni.
Ili kutekeleza vipaumbele hivyo,Ofisi hiyo na taasisi zilizo chini yake imeomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi Bilioni 148.62 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli zake kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026.