Habari
PROF. MKUMBO ATEMBELEA NA KUKAGUA KIWANDA CHA MVINYO CHA ALKO VINTAGE, DODOMA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), amefanya ziara katika Kiwanda cha Alko Vintage na kumtia Moyo Mwekezaji wa ndani akisema Serikali inathamini uwekezaji wake, hasa katika kuzalisha ajira, kukuza uchumi wa nchi, na kuchangia katika Pato la Taifa.
Prof. Mkumbo ameyasema hayo Juni Mosi 2024 Jijini Dodoma wakati alipotembelea kiwanda cha Mvinyo kinachomilikiwa na mtanzania ambapo ameongeza kuwa uwekezaji uliofanyika katika kiwanda hicho ni takribani zaidi ya bilioni 13.
“Tutaendelea kuhamasisha matumizi ya malighafi za ndani ili zisije zikakosa soko la watumiaji pia tutaqngalua na masoko ya nje ya nchi maana masoko yakiwepo zile malighafi za ndani hazitakosa wanunuzi na wawekezaji wengi watakuja kufungua viwanda”, amesema Prof. Mkumbo.
Prof. Mkumbo ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ikiwemo hatua za kikodi walizoziweka kwa mwaka huu ambazo zinalenga kukuza viwanda vya ndani, kusukuma mauzo ya nje kwa bidhaa zinazozalishwa ndani na kuwapa mazingira mazuri wawekezaji ili waendelee kuwekeza nchini.
Ameongeza kuwa Serikali inahitaji kuona mwekezaji anakuwa na sehemu ya kuuza bidhaa zake ndiyo maana tunaendelea kushirikiana nao kwasababu bidhaa wanazozizalisha zinakubalika ndani na nje ya nchi kama China na kwingineko na hatua inayofuata ni kutafuta soko Ulaya kwamaana bidhaa ikishaingia huko imekubalika dunia nzima.
“Lakini tuna fursa ya soko kubwa la Afrika hili ambalo tumekuwa tukilizungumza maana yake Afrika tuna soko la Bilioni 1.4 kwahiyo mwekezaji huyu tutaendelea kumshawishi ili aweze kupeleka bidhaa zake katika mataifa mengine zaidi ndani ya bara letu hili la Afrika”,ameongeza Prof. Mkumbo.
Pia amesema wanatambua kuwa viwanda ndiyo njia sahihi ya kuharakisha maendeleo ya uchumi wa nchi lakini ni muhimu sana kwenye kukuza ajira kwa vijana na dunia kwasasa ina vijana wengi wanaomaliza vyuo mbalimbali kwahiyo hiyo ni njia nzuri ya kusukuma ajira kupitia viwanda.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Alko Vintage Bw. Archard Kato amesema kwasasa wanauza Mvinyo wao katika masoko yote ya Afrika Mashariki pamoja na China hiyo ikiwa ni namna ya wao kukuza masoko yao ambapo Julai 5, 2024 wataenda kufanya ufunguzi rasmi na kuanza uzalishaji pamoja kuingia mkataba wa kuanza kuuza Amerika.
“Lengo letu sisi ni kwenda kwenye masoko ya nje kwasababu tuna utaalamu wa kutosha na teknolojia za kutosha na rasilimali watu tunayo ya kutosha tukishirikiana nao katika kuhakikisha yote yanaenda vizuri vilevile na ubora wa Mvinyo unaenda vizuri “, amesema Bw. Kato.