Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

PROF. MKUMBO ATETA NA BODI NA MENEJIMENTI ZA TIC NA EPZA


Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, amezitaka Bodi na Menejiment za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Maeneo ya Uzalishaji ya Mauzo ya Nje (EPZA kuchangia ipasavyo katika mapendekezo ya muundo na majukumu ya taasisi.

Prof. Mkumbo ametoa wito huo Mei 03, 2024 alipofanya kikao na Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi pamoja na Memejimenti za TIC na EPZA kilocholenga kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa maamuzi ya Serikali ya kuunganisha taasisi hizo mbili.

''Kachangieni ipasavyo katika mapendekezo ya muundo na majukumu ya taasisi mpya, zingatieni changamoto zilizopo sasa ili kuwa na taasisi imara itakayovutia uwekezaji" Alisema Prof. Mkumbo. 

Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaamu, Mhe. Mkumbo alieleza kwamba kikao hicho, pamoja na mambo mengine kililenga kuhakikisha Bodi na Menejimenti za taasisi hizo mbili zinashirikishwa ipasavyo katika utekelezaji wa maamuzi ya Serikali.

Katika taarifa yake,  Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida, maamuzi ya kuunganisha taasisi hizo mbili yalikuwa matokeo ya  tathmini ya mwaka 2023 ya utendaji wa Mashirika na Taasisi za Umma kwa lengo la kubaini uwepo wa taasisi zenye muingiliano wa kimajukumu, na taasisi ambazo malengo ya kuanzishwa kwake yamepitwa na wakati au uendeshaji wake kukosa tija kwa lengo la  kutafuta namna bora ya kuboresha.

Tathmini hiyo pamoja na mambo mengine, ilibaini kuwa, majukumu ya taasisi takribani 22 ikiwemo EPZA na TIC yanashabihiana na kuelekeza taasisi hizo mbili ziunganishwe na kuunda taasisi moja. 

Dkt. Kida alieleza kwamba, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, iliunda Kamati ya Wataalamu wa Serikali kufanya uchambuzi na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya kuunganisha TIC na EPZA ikiwa ni pamoja na mapendekezo ya kutunga Sheria mpya ya Uwekezaji ambayo,  pamoja na mambo mengine itawezesha kuanzishwa kwa taasisi hiyo mpya.