Habari
Prof. Mkumbo awahimiza wawekezaji nchini kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kwa kuyachakata na kuuza bidhaa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb,) amewahimiza wawekezaji katika viwanda mbalimbali nchini kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kwa kuyachakata hadi kuwa bidhaa ili kukuza uchumi wa Nchi.
Mhe. Prof. Mkumbo ameyasema hayo Juni 29, 2024 alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa kiwanda kipya cha kuchakata mbegu ya alizeti cha Wild Flower Grains & Oil Mills Company Limited pamoja na kiwanda cha kuchakata pamba cha Bio Sustain company limited vilivyopo Mkoani Singida ili kukagua maendeleo ya viwanda hivyo na kusikiliza changamoto zao.
Mhe. Prof. Mkumbo amewapongeza wawekezaji hao kwa kazi nzuri wanayofanya ya uwekezaji katika viwanda kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha viwanda vyetu vinachakata mazao ya kilimo ili kuinua uchumi wa Nchi na kuongeza ajira kwa wanachi wetu.
“Kiwanda hiki cha Wild Flower Grains & Oil Mills Company Limited kitakapokamilika kitatoa ajira za moja kwa moja zaidI ya 190 na zisizo za moja kwa moja Zaidi ya 400 na wakulima Zaidi ya 26,000 watanufaika na mradi huu, na wakulima hawa ni wanufaika wa jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambapo amesaidia kuongeza uzalishaji wa alizeti kutoka tani laki nne hadi milioni moja hivyo kupitia mradi huu wakulima wetu wa alizeti wamepata soko la uhakika” amesema Prof. Mkumbo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Godwin Gondwe akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendegu amesema kuwa viwanda hivi vimekuwa ni msaada mkubwa katika Mkoa wa Singida hasa katika kutoa ajira kwa wananchi wa Singida na mikoa jirani, kusaidia jamii hasa katika ujenzi wa madarasa na mabweni, ukarabati wa miundombinu, ujenzi wa vituo vya afya na kujenga vituo vya maji kwa ajili ya magari ya zimamoto.
Awali akitoa taarifa ya kiwanda cha Wild Flower Grains & Oil Mills Company Limited Bw. Khalid Ally Omary amesema kuwa ujenzi wa kiwanda umefikia asilimia 95 kukamilika ambapo kwa sasa wapo katika hatua za majaribio.
Naye Mkurugenzi wa kiwanda cha Bio sustain T. Limited Bw. Sajjad Haider Ghulam amesema kuwa kiwanda chao kinafanya kazi ya kuchakata pamba kwa kupokea malighafi kutoka kwa wakulima.
Mhe. Mkumbo amewakikishia wawekezaji hao kuwa Serikali inatambua mchango wao mkubwa katika kutengeneza ajira na kukuza uchumi wa Nchi hivyo serikali itahakikisha inawasikiliza na kutatua changamoto zao ili viwanda hivi viendelee kuwepo na kuendelea kuwa msaada kwa Nchi yetu.