Habari
PROF. MKUMBO: NCHI IMEPIGA HATUA KUBWA TANGU UHURU

Tanzania imepiga hatua kubwa za maendeleo tangu ilipopata Uhuru miongo sita iliyopita, ambapo kila awamu ya uongozi imetoa mchango wake mkubwa. Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi (OR-MU), Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb.), alipokuwa akihutubia kwenye kongamano la kiuchumi lililofanyika leo Mei 3, 2025, jijini Arusha.
Mhe. Prof. Mkumbo alisema kuwa awamu ya kwanza ilijenga msingi wa taifa, ikijenga miundo mbinu ya kuhifadhi usalama na maendeleo ya nchi.
Awamu ya pili ilifungua sekta binafsi, ikiwapa wananchi nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi. Awamu ya tatu ilijenga taasisi za kusimamia sekta binafsi, huku awamu ya nne ikizidisha juhudi za kuielimisha sekta hiyo kwa lengo la kuimarisha biashara na uwekezaji.
Awamu ya tano ilijenga miundombinu ya kitaifa kwa kuimarisha miundombinu na huduma za kijamii, na sasa, awamu ya sita inahakikisha nchi inakuwa na taswira inayovutia wawekezaji wengi zaidi na kukuza Uchumi wa Nchi.
Mhe. Prof. Mkumbo alibainisha kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta mbalimbali. Pato la taifa liliongezeka kutoka dola za kimarekani bilioni 13.3 mwaka 2000 hadi dola bilioni 86 mwaka 2024, huku pato la mtu mmoja likiongezeka kutoka dola 280 hadi dola 1,232.
Kampeni za kupambana na umaskini zimezaa matokeo, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa asilimia kubwa kwa umaskini ule uliokithiri kutoka 36% mwaka 2000 hadi 26% mwaka 2022.
Aidha, vifo vya akina mama wakati wa kujifungua vimepungua kwa kiasi kikubwa, kutoka 750 kwa kila akina mama 100,000 mwaka 2000 hadi 104 mwaka 2022.
Sekta za maji na elimu nazo zimefanyika maboresho makubwa, kutoka asilimia 32 hadi 77 kwa vyanzo vya maji vijijini, huku zaidi ya asilimia 97 ya watoto wakijiandikisha kwenye elimu ya msingi kwa mwaka zaidi.
Mwelekeo wa maendeleo ya kiuchumi na uwekezaji katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeonyesha kuwa Tanzania inalenga kujenga uchumi wa dola trilioni 1 ifikapo mwaka 2050, kwa kuhimiza sekta binafsi kuendelea kuchangia kwa bidii kwenye ukuaji wa pato la taifa na la mtu mmoja mmoja.
Mhe. Prof. Mkumbo alihitimisha kwa wito kwa sekta binafsi kuacha ujanja-janja na badala yake kufanya biashara kwa kuwa na uzalendo wa kulipa kodi halali, kwani kodi ndiyo nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.