Habari
RAIS SAMIA AWEKA REKODI KURATIBU UANDISHI WA DIRA ISIYOKUWA NA ITIKADI ZA KISIASA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amebainisha kuwa Rais wa awamu wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Kiongozi Mkuu wa Pili wa Tanzania kufanikisha uandishi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Kulingana na Waziri Kitila Mkumbo wakati wa Uzinduzi wa Dira hiyo leo Julai 17, 2025 Mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Jijini Dodoma kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, amebainisha kuwa Rais wa kwanza kufanya hivyo alikuwa Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamin William Mkapa mnamo mwaka 2000.
"Huko nyuma na kabla ya kuwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 hatukuwa na mpango wa maendeleo ulioitwa Dira, hii haimaanishi nchi yetu ilikuwa inaongozwa bila Dira, la hasha kwa hakika tulikuwa na Dira katika mipango yetu ya maendeleo; kwa mfano Azimio la Arusha mwaka 1967 lililoasisiwa na Mwalimu Nyerere, lilikuwa Dira kamili ya nchi yetu ambayo iliongoza mipango ya nchi hii kwa miongo mitatu." Amesema.
Aidha Prof. Mkumbo amebainisha kuwa kwa awamu ya Pili ilikuwa na Programu ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 1987-2002 chini ya Uongozi wa Hayati Ali Hassan Mwinyi ambayo iliiongoza Tanzania katika maendeleo kabla ya kuanza kwa Dira ya kwanza isiyoegemea kwenye Itikadi za Vyama vya siasa nchini Tanzania.