Habari
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan awakaribisha wawekezaji kutoka India.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewakaribisha wawekezaji kutoka India kuja Tanzania kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Viwanda, Kilimo, Uvuvi na uongezaji thamani, Afya, Madini, Tehama, Utalii, Benki na Miundombinu.
Mhe. Rais ameyasema hayo tarehe 10 Oktoba, 2023 jijini New Delhi katika Kongamano la Biashara lililowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka India na Tanzania na kuwahakikishia mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini.
Katika Kongamano hilo, Waziri Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa nchi ya India imeendelea kuwa mshirika wa kimkakati wa Maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania, Aidha, ameongeza kuwa biashara kati ya Tanzania na India imeendelea kukua.
Prof. Mkumbo ameongeza kuwa ziara ya Mhe Rais nchini india itaongeza na kukuza biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi mbili na pia ziara hiyo imeipa fursa Tanzania kujifunza maendeleo makubwa ya kiuchumi yaliyopelekea kufanikiwa kwa nchi ya India.