Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

SERIKALI YAJA NA FURSA TANO (5) ZA UWEKEZAJI KWA VIJANA


Katika hatua itakayobadilisha taswira ya ajira na uwekezaji kwa vijana nchini, Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji (OR MU), Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) imetangaza fursa tano (5) mahsusi za uwekezaji na uwezeshaji kwa vijana.

Prof. Mkumbo ametoa taarifa hiyo leo tarehe 8 Disemba, 2025 alipozungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kuhusu vipaumbele na fursa kwa vijana katika miaka mitano ijayo, fursa hizo zinalenga kuwawezesha kuwa wamiliki wa viwanda na wafanyabiashara wakubwa.

“Hatua hii ni sehemu ya mkakati mpana wa Taifa wa kuzalisha ajira milioni nane (8) na kuvutia uwekezaji wa dola za Kimarekani Bilioni 50 ifikapo mwaka 2030” Alisema Prof Mkumbo.

Aidha, Waziri ameeleza kuwa Serikali inatambua vijana kama nguzo muhimu ya uchumi na inalenga kuwaweka mstari wa mbele katika safari ya maendeleo, na kutaja fursa hizo tano kuwa ni;

Kituo Maalum cha Vijana (YIRC): Kuanzishwa kwa Youth Investors Resource Centre (YIRC) kabla ya mwisho wa mwaka, kutoa ushauri, mafunzo, na uelekezi kwa wawekezaji vijana.

Programu Kabambe ya Viwanda: Programu ya kuwawezesha wahitimu wa vyuo kuanzisha viwanda, ikijumuisha mafunzo, kuunganishwa na mitambo, malighafi, na Mikopo kupitia benki washirika (Azania, TCB, CRDB).

Ardhi Maalum kwa Vijana: Serikali imetenga maeneo makubwa ya ardhi kwa miradi ya viwanda ya vijana, ikiwemo Dodoma (Nala - Ekari 100), Pwani (Kwala - Ekari 20), Mara (Bunda - Ekari 100), Ruvuma (Songea - Ekari 100) na Bagamoyo (Ekari 20).

Majengo ya Viwanda ya Kukodisha (Industrial Sheds): TISEZA itashirikiana na sekta binafsi kujenga majengo ya viwanda yatakayokodishwa kwa gharama nafuu kwa Watanzania. Hatua hii itapunguza mzigo wa gharama za ujenzi.

Huduma za Uwekezaji Kufika Kila Mkoa (2028): Huduma za TISEZA zitasogezwa kila mkoa ili kurahisisha vijana kupata taarifa na usaidizi popote nchini, kutekeleza agizo la Mhe. Rais.

Mbali na fursa hizi, Serikali inaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na inakamilisha mikakati ya utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 na maboresho ya Mashirika ya Umma.