Habari
SERIKALI YATANGAZA MIKAKATI 8 YA KUVUTIA UWEKEZAJI, INAYOWEKA KIPAUMBELE KWA VIJANA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, ametangaza mikakati nane (8) ya kukuza uwekezaji nchini, inayoweka kipaumbele kwa vijana na ajira.
Prof. Mkumbo ametangaza mikakati hiyo muhimu leo Novemba 28, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA).
Katika hafla ya uzinduzi wa bodi hiyo iliyohudhuriwa na Naibu Waziri Mhe. Dkt. Pius Chaya na Katibu Mkuu Dkt. Taus M. Kida pamoja na viomgozi wengine, Mheshiwa Waziri ameeleza kuwa mikakati hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kusogeza huduma za uwekezaji karibu na wananchi.
"Tunataka uwekezaji unaojibu shida za wananchi, hususan kutoa fursa zaidi kwa vijana," alisema na kutaja mikakati hiyo ambayo ni;
i. Kuanzisha Kituo Maalimu cha Wawekezaji Vijana: Kuanzisha Youth Investors Resource Centre (Mabibo, Dar es Salaam) kutoa mafunzo na usaidizi kwa vijana, na kuwa na uwakilishi nchi nzima kupitia TISEZA.
ii. Kuanzisha Programu ya Ardhi na Viwanda kwa Vijana: Kuanzisha programu maalum ya kuwapa vijana waliomaliza vyuo maeneo maalum (mfano, Dodoma-Nala, Pwani-Kwala, Mara-Bunda) kuwekeza kwenye viwanda.
iii. Kusogeza Huduma za Uwekezaji Kila Mkoa: Kusogeza huduma za TISEZA kufikia kila Mkoa ifikapo 2028 kwa kuanzisha vituo maalum vya uwekezaji.
iv. Ubia wa Miundombinu: TISEZA kuingia ubia na sekta binafsi kujenga majengo ya viwanda (industrial sheds) ya kukodisha kwa gharama nafuu.
v. Vivutio Vipya: Kuanzisha vivutio vipya vya uwekezaji mara kwa mara na kuwakaribisha wawekezaji kutoa maoni ya kuboresha sheria.
vi. Jukwaa la Makutano: Kuanzia Januari 2026, Prof. Mkumbo atakutana na wawekezaji kila miezi mitatu kujadili na kutathmini mwenendo wa uwekezaji.
vii. Kongani ya Viwanda Bagamoyo: Kuweka kipaumbele cha kuendeleza eneo la kiuchumi Bagamoyo ili kuanzisha kongani ya viwanda itakayolenga soko la ndani na nje, kujiandaa kwa Bandari ya Bagamoyo.
viii. Viwanda vya Bidhaa za Nje: Kuvutia uwekezaji katika kuzalisha bidhaa ambazo nchi inaagiza kwa wingi.
