Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

Tahtimini yaonesha Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia sita (6) kwa mwaka katika kipindi cha miaka ishirini (20) iliyopita.


Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo wakati wa kuwasilisha bungeni mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2024/2025.
 
Prof. Mkumbo amesema uchumi wa Tanzania ulionesha hali kubwa ya ustahimilivu hata katika kipindi cha misukosuko mikubwa ya kiuchumi duniani, ikiwemo wakati wa janga la ugonjwa wa UVIKO-19 na vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.
 
"Aidha, katika kipindi cha miaka 20 iliyopita aina ya bidhaa tunazouza nje na nchi tunazofanya nazo biashara zimebadilika sana." 
"Miaka 20 iliyopita tuliuza zaidi mazao ya kilimo wakati sasa mauzo yetu ya nje yanatawaliwa zaidi na mauzo ya madini."
 
Amesema miaka 20 iliyopita Tanzania iliuza zaidi bidhaa zetu katika masoko ya Ulaya, Marekani na Afrika, lakini kwa sasa tunauza zaidi katika masoko ya nchi za Asia (China, India, n.k.), Afrika na Mashariki ya Kati.
 
"Taarifa ya Benki ya Dunia ya Septemba 2023 kuhusu uchumi wa Tanzania, uchumi wa Tanzania umeendelea kuhimili vyema athari za UVIKO-19 na changamoto zingine za dunia zilizojitokeza katika miaka mitatu iliyopita."
 
Amesema pamoja na changamoto zilizojitokeza uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa mageuzi makubwa yaliyolenga katika kuchochea na kuimarisha ushindani katika uchumi.
 
Pia kuendelea kuboresha na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini na kuendelea kuaminiwa na taasisi za fedha duniani, pamoja na wadau wetu wa maendeleo.