Habari
TANZANIA, EU KUIMARISHA USHIRIKIANO WA BIASHARA NA UWEKEZAJI KUELEKEA DIRA 2050
Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hayo yamejadiliwa katika majadiliano yaliyowakutanisha wawakilishi wa nchi wanachama wa EU, Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, jumuiya za wafanyabiashara wa Ulaya pamoja na taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali jijini Dar es Salaam Agosti 26, 2026.
Miongoni mwa taasisi zilizoshiriki ni Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), ambazo zina mchango mkubwa katika kuwezesha biashara na uwekezaji nchini.
Akifungua majadiliano hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa mkutano huo, amesema jukwaa hilo limetoa fursa kwa pande hizo kutathmini hatua zilizopigwa katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, huku zikibainisha changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka.
Mhe. Prof. Mkumbo amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kujenga mazingira rafiki na yenye ushindani kwa wawekezaji, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuvutia uwekezaji wenye tija unaochochea ukuaji wa uchumi na kuleta manufaa kwa Taifa na wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, amesema Wizara itaendelea kutekeleza jukumu lake la kuwa kiungo kati ya wawekezaji na wafanyabiashara wa kimataifa na mamlaka husika nchini ili kuhakikisha biashara na uwekezaji wa kimataifa vinachangia kikamilifu katika malengo ya maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wa EU, Wenyeviti Wenza wa majadiliano hayo, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mhe. Anne-Sophie Avé, na Balozi wa Ireland, Mhe. Nicola Brennan, wameeleza utayari wa Umoja huo kuendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo wa Tanzania, huku biashara na uwekezaji vikipewa nafasi kubwa katika kuchangia utekelezaji wa Dira 2050.
Majadiliano hayo yanafuatia ‘Political Dialogue’ kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya iliyofanyika Juni 2026.
