Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

PROF. MKUMBO AONGOZA UJUMBE ZIARA YA UWEKEZAJI NIGERIA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, ameongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa Serikali ya Tanzania katika ziara ya kimkakati jijini Lagos, Nigeria, kutembelea Kampuni za Dangote.

Katika ziara hiyo, Prof. Kitila amefanya mazungumzo ya kimkakati na Rais na Mtendaji Mkuu wa Dangote Group, Alhaj. Aliko Dangote, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa uwekezaji kati ya Tanzania na kampuni hiyo kubwa zaidi ya viwanda barani Afrika.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa kutafsiri maono ya DIRA 2050 ambayo imesema Sekta Binafsi ndiyo iwe injini ya kujenga uchumi katika safari ya kulifikia Taifa lanye uchumi wa dola za Marekani Trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Pia ziara hiyo ni mwendelezo wa ushirikiano unaozidi kuimarika kati ya Serikali ya Tanzania na Dangote Group, kufuatia ziara ya hivi karibuni ya Alhaj Dangote nchini Tanzania ambapo alikutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kufanya mazungumzo kuhusu kupanua uwekezaji katika sekta mbalimbali za kimkakati za uchumi.

Mazungumzo hayo yaliweka msingi wa kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi na kuharakisha maendeleo ya viwanda nchini Tanzania huku ziara ya Lagos ikiwa ni hatua inayofuata ya kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa Dar es Salaam kupitia miradi ya uwekezaji na ushirikiano wa muda mrefu.

Mbali na Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, ujumbe huo unajumuisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya.

Wengine ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum (TISEZA), Balozi, Dkt. Aziz Mlima, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gillard Teri, viongozi wandamizi serikalini na watengaji wakuu wa mashirika mbalimbali ya kwenye sekta za uchukuzi, usafirishaji, ugavi (logistics), bandari na miundombinu.