Habari
TANZANIA NA UINGEREZA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA KUKUZA UWEKEZAJI.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, ameongoza ujumbe wa Kibiashara na Uwekezaji wa Tanzania jijini London chini Uingereza.
Ujumbe huo uliojumuisha sekta ya Umma na Binafsi umeandaliwa kwa ushirikiano na Serikali ya Uingereza kwa lengo la kuvutia uwekezaji na mitaji kutoka Uingereza katika sekta mbalimbali nchini.
Pamoja na mambo mengine, Ujumbe huo ulishiriki katika Kongamano la Uwekezaji na Biashara kati ya Uingereza na Tanzania ambapo Dkt.Kida alieleza hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara nchini na kubainisha baadhi ya hatua mahsusi zilizofanyika kuwa ni Uwepo wa Sheria mpya ya Uwekezaji ya Mwaka 2022 ambayo pamoja na masuala mengine imeweka mazingira bora kwa wawekezaji ikiwemo kuimarisha mifumo ya kitaasisi katika uratibu, ulinzi, uvutiaji, uhamasishaji na uwezeshaji wa uwekezaji nchini kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, alieleza kuwa Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kuhamasisha Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imeendelea kutoa vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kwa wawekezaji wanaowekeza katika sekta mbalimbali nchini, huku akieleza kuwa Uingereza ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa nchini ambapo kwa mujibu wa takwimu za TIC kuanzia mwaka 1997 jumla ya miradi 966 imesajiliwa yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 5.58. Aidha, alieleza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha uwekezaji kutoka Uingereza unafikia Dola za Marekani Bilioni 10 kufikia mwaka 2030.
Katika ujumbe huo, Katibu Mkuu aliambatana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Habiba Omar pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Bw. kheri Mahimbali. Aidha Wizara na taasisi zingine za Serikali zilizoshiriki katika ujumbe huo ni pamoja na Wizara ya Kilimo, Fedha, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Uchukizi, pamoja na TIC, ZIPA, ATCL ,TANESCO,TAFICO.