Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

TISEZA YAZINDUA MAENEO MAALUM YA KIUCHUMI


Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imezindua rasmi Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs) leo, tarehe 12 Agosti 2025 jijini Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kuvutia uwekezaji mkubwa wa viwanda na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji barani Afrika.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila A. Mkumbo alisema tangu kuanzishwa kwa TISEZA, Serikali imeendelea kuimarisha uwekezaji katika SEZs kwa kuziunganisha na miradi mikubwa ya miundombinu kama vile Reli ya Kisasa (SGR), barabara kuu, bandari na viwanja vya ndege.

Prof. Mkumbo alitaja maeneo matano ya kimkakati yanayotangazwa kwa uwekezaji kuwa ni Nala SEZ (Hekta 607), Kwala SEZ (Hekta 40.5 – ekari 100), Buzwagi SEZ (Hekta 1,333), Bagamoyo Eco Maritime City – BEMC SEZ Awamu ya Kwanza (Hekta 151) na Benjamin William Mkapa SEZ (Upanuzi) yenye mita za mraba 13,000.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, alisema kuwa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji Uwekezaji katika SEZs ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi kupitia ajira, mauzo ya nje, uhamisho wa teknolojia na ubunifu wa viwanda.

Dkt. Kida aliongeza kuwa kuunganisha SEZs na miundombinu mikubwa ya kimkakati kama SGR, bandari na viwanja vya ndege kutajenga msingi imara wa mageuzi ya kiuchumi yatakayogusa kila mkoa wa Tanzania.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Bw. Giread Teri, aliwataka wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje ya nchi kuchangamkia fursa za kuanzisha viwanda nchini, akibainisha kuwa serikali inatoa maeneo bure kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.

“Waje wazalishe kwa soko la ndani, soko la Afrika Mashariki na hata kuuza nje ya bara. Vivutio vingi vimetolewa na serikali na leo tumeyazindua rasmi,” alisema Bw. Teri.

Maeneo haya ya kimkakati yanatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa Taifa ikiwemo ajira kwa maelfu ya vijana, kuongeza mauzo ya nje, kupunguza uagizaji bidhaa na kuhamisha teknolojia mpya za viwanda nchini.