Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

UWEKEZAJI KATIKA HATUA MPYA: TISEZA YAASISIWA KUFUATIA MABADILIKO YA KISHERIA


Mwezi Julai, 2025 utaweka katika kumbkumbu za historia ya mapinduzi ya kimuundo katika sekta ya uwekezaji nchini Tanzania, hii inafuatia kuanza kutumika rasmi kwa Sheria ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi, Na. 6 ya Mwaka 2025. 

Kuanzishwa kwa sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Februari 13, 2025, na kupata idhini ya Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kunafungua ukurasa mpya katika kuvutia, kuratibu na kulinda mitaji huku ikibeba dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. 

Kuanzishwa kwa TISEZA: 
Aidha, kuanza kutumika kwa Sheria hiyo, kuanzisha rasmi Mamlaka mpya yenye nguvu ya kusimamia masuala yote yahusuyo uwekezaji ‘Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania’ (Tanzania Investment and Special Economic Zones Authority - TISEZA).
Mamlaka hiyo, TISEZA imezaliwa kutokana na kuunganishwa kwa majukumu muhimu yaliyokuwa yakitekelezwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), muunganiko huo unalenga kuunda taasisi moja imara na yenye ufanisi wa hali ya juu.
Hatua ya uanzishwaji wa Mamlaka hiyo, ilikwenda sambaba na uteuzi wa Bw. Gilead John Teri aliyeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa TISEZA. 

Dhamira na Malengo: 
Malengo makuu ya Mamlaka hii mpya ni pamoja na:
i)    Kuweka mfumo wa kitaasisi kwa ajili ya uratibu, ulinzi, uvutiaji, uhamasishaji na uwezeshaji wa uwekezaji nchini.
ii)    Kuweka masharti ya uendelezaji wa uwekezaji na mazingira bora yanayotarajiwa kupunguza urasimu kwa wawekezaji wa ndani na nje.
iii)    Kuendeleza na kusimamia kwa ufanisi maeneo maalumu ya kiuchumi.
Kuanza kutumika kwa Sheria Na. 6 ya 2025 na uanzishwaji wa TISEZA ni dhihirisho la azma ya dhati ya Serikali katika kuboresha 'hali ya ushindani wa uwekezaji' nchini. 

Maboresho haya ya kimkakati yanatarajiwa kutoa dira thabiti, kuondoa vizuizi vya utekelezaji, na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa na midogo katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi. Ni matumaini ya Serikali kwamba TISEZA itakuwa chachu ya kuvutia mitaji mipya na kujenga ajira nyingi zaidi kwa Watanzania.