Habari
UWEKEZAJI WA WABIA WAIMARISHA UFANISI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb), ametembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na kuridhishwa na maboresho katika uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Katika ziara yake aliyoifanya leo Oktoba 21, Mhe. Prof. Mkumbo ameipongeza TPA kwa usimamizi wa uwekezaji wa kimkakati wa wabia wa kimataifa, DP World na East Africa Gateway Terminal Ltd (EAGTL), ulioleta miundombinu ya kisasa na kuongeza ufanisi wa huduma.
Akitaja baadhi ya mafanikio ya maboresho hayo, Mhe. Prof. Mkumbo amesema yamechangia kupungua kwa muda wa kuhudumia meli kutoka siku saba hadi kufikia siku tatu hadi nne, huku idadi ya siku za kusubiri kwa meli bandarini zikipungua kutoka siku 30 hadi kufikia siku tano hadi saba.
“Maboresho haya ni muhimu kwa maendeleo ya taifa na yanatarajiwa kuchangia moja kwa moja katika Pato la Taifa” Amesisitiza Mhe. Mkumbo.
Aidha, Mhe. Waziri Prof. Mkumbo amewataka wawekezaji wa Terminal 1 na 2, DP World na EAGTL, kuhakikisha wanatekeleza kikamilifu makubaliano yao ili kuleta tija kwa nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa, amesema kuwa uwekezaji wa miundombinu ya kisasa umeongeza ufanisi mkubwa katika Bandari ya Dar es Salaam, hatua inayosaidia kuimarisha biashara za kimataifa na kuvutia wawekezaji zaidi.
Mafanikio ya uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam, yanaweka misingi imara wa ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya bandari, ambayo ni sehemu muhimu ya usafirishaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi.