Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

WAKUU WA MIKOA WAHIMIZWA KUHAMASISHA WANANCHI NA WADAU MBALIMBALI KUTOA MAONI YA DIRA 2050


Wakuu wa Mikoa wameagizwa kuhamasisha wananchi na wadau mbalimbali kutoa maoni ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ili kusaidia timu ya kukusanya maoni kupata maoni yatakayoakisi mahitaji halisi ya wakati.

Agizo hilo limetolewa tarehe 17 Aprili, 2024 na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipofungua semina kwa Wakuu wa Mikoa kuhusu Majukumu yao katika Mchakato wa Kutoa maoni ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 au zaidi.

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri Mkuu, ametoa maagizo mahususi yaliyowataka Viongozi hao kushiriki kutoa maoni na kusaidia uratibu ili timu ya ukusanyaji wa maoni ifanye kazi yake kwa ufanisi kwa kuwa viongozi hao wanawafahamu vyema wananchi wao. "Mshirikishe ngazi mbalimbali zilizo chini yenu, Wakuu wa Wilaya, Kata mpaka vitongoji" 

Aidha, alisisitiza kuwa, viongozi hao walipe kipaumbele suala la  ushirikishwaji wa wananchi wote. Maagizo mengine, ni kuhakikisha zoezi la ukusanyaji wa maoni linafanyika kwa amani na utulivu.

Pamoja na maagizo hayo, Mhe. Kassim Majaliwa ameitaka Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kuhakikisha inaendelea kutoa elimu kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo kwa njia ya vyombo vya Habari.

Vile vile, ameagiza kuhakikisha makundi mbalimbali hayasahauliki hasa viongozi wa Dini, ambapo ameshauri waombwe kuwakumbusha waamini wao kuhusu umuhimu wa kutoa maoni.

Mhe. Waziri Mkuu amesisitiza kuwa timu ya ukusanyaji wa Maoni iwafikie makundi maalumu ikiwemo walemavu wasioweza kufika kwenye mikutano na makongamano kwa kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anatoa maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 au zaidi.