Habari
WAWAKILISHI WA SERIKALI KWENYE MASHIRIKA YA KIMATAIFA WATAKIWA KUZINGATIA AJENDA ZA TAIFA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, amewataka wawakilishi wa nchi kwenye ngazi za uongozi za mashirika yenye hisa chache za Serikali kufahamu ajenda ya nchi ili kuhakisha wanalinda maslahi ya Taifa.
Prof. Mkumbo ametoa wito huo alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wawakilishi wa nchi katika makampuni hayo yaliyoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.
"Nyie mnatuwakilisha kule, na makampuni mengine ni ya kimataifa, yana uwezo, uzoefu na ujanja wa kuendesha biashara duniani, menejimenti zao zinaweza kuwa na wataalamu wenye uzoefu na uwezo mkubwa", aliwatahadharisha Prof. Mkumbo.
Prof. Mkumbo aliwasisitiza kusoma nyaraka na inapobidi kutafuta wataalamu wa kuwasaidia kuzichambua ili watoe uwakilishi wenye maanufaa kwa Taifa.
Aliwataka kufahamu kuwa wapo katika makampuni hayo kumuwakilisha mwenye hisa amabaye ni Serikali hivyo kabla ya kukaa kwenye kikao cha uwakilishi, ni vyema mkarejea kwa mwenye mali ambaye ni Serikali na kufahamu ajenda yake mahususi kuhusu sekta husika.
Prof. Mkumbo alifafanua kuwa moja ya ajenda katika ajenda ya uchimbaji wa madini ya kimkakati inayolenga kuhakikisha hayasafirishwi yakiwa ghafi ilivyo mwiba kwa wamiliki wa makampuni ya uchimbaji hivyo wasipokuwa makini wanaweza kupotoshwa juu ya msimamo wa nchi.
"Ni rahisi sana kwenda kuelezwa kuhalalisha kwanini hilo haliwezekani, na wewe unakuja kutueleza sisi Serikali kwamba hilo haliwezekani, kwa hiyo badala ya kusukuma ajenda yetu kule, unatumika kuwa wakala bila kujua", alitahadharisha Prof. Mkumbo.
Aidha, alisema kuwa angependa kuona makampuni yanayokuja kufanya kazi Tanzania yawe ya Kitanzania kwa kuwa na utambulisho wa Kitanzania, tofauti ilivyo kwa makampuni mengi yaliyosalia na tamaduni za nchi yanakotoka.
"Mna nafasi ya kuhakikisha makampuni hayo yanapata utambulisho wa Kitanzania katika tabia na utendaji" Alisisitiza Prof. Mkumbo.
Pia Prof. Mkumbo aliwataka kujifunza ujuzi wa kiutendaji, tabia njema za namna bora ya kuendesha makampuni ya yanayomilikiwa na Serikali, pamoja na kutoa mrejesho kwa Serikali na kuongeza thamani, ili hatimaye Serikali ipate thamani ya uwekezaji unaofanywa na makampuni hayo nchini.
"Kwa sasa ajenda ya Serikali ni kuongeza thamani kwenye kila mazao yanayozalishwa nchini, iwe madini, iwe kilimo tunataka kuona ongezeko la thamani, na vile vile kupunguza uingizaji wa bidhaa zinazoweza kupatikana nchini" Alisisitiza, Prof. Mkumbo.